Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je Afrika ni tishio kubwa? Ahoji Rais Mutharika

Profesa Arthur Peter Mutharika, Rais wa Malawi wakati akihutubia mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani
UN/Cia Pak
Profesa Arthur Peter Mutharika, Rais wa Malawi wakati akihutubia mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani

Je Afrika ni tishio kubwa? Ahoji Rais Mutharika

Amani na Usalama

Malawi imesema inaunga mkono msimamo wa Afrika wa kutaka kuwepo kwa wajumbe wawili wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na 5 wasio na kura turufu.

Rais Arthur Peter Mutharika wa Malawi ametoa msimamo huo wa Malawi wakati akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, wakati huu ambapo hoja ya kuongeza au kupunguza idadi ya nchi 5 zenye kura turufu ndani ya baraza hilo imekuwa ikisuasua kila uchaao.

Hivi sasa Baraza hilo la Usalama lina nchi 5 zenye ujumbe wa kudumu ambazo ni  China, Marekani, Ufaransa, Uingereza na Urusi ambapo Rais huyo wa Malawi amehoji, “kwa nini baadhi ya mataifa yawe na hofu ya kupoteza uthabiti wao kwa kuweka nafasi zaidi kwa Afrika, ilhali hupunguzi madaraka kwa kujumuisha mataiga mengine 10. Je Afrika ni tishio kubwa?”.

Rais Mutharika akaenda mbali akisema kuwa “huu ubaguzi wa Afrika lazima ukome. Kwa nini tunaruhusu shirika hili linalotuhumiwa kwa unafiki- yaani sisi tunahubiri demokrasia kila pahali ilhali sisi wenyewe hatuna demokrasia ya kutosha kujumuisha bara ambalo ni karibu theluthi moja ya wanachama wa chombo hiki?”

Ametaka Umoja wa Mataifa uishi maudhui ya mwaka huu ya Baraza hilo Kuu ya ujumuishi akisema kuwa, “ hatuwezi kuzungumzia uwajibikaji wa pamoja ilhali tunaengua Afrika na tunainyika haki yake ya kushiriki kwenye maamuzi. Hatuwezi kuzungumzia uongozi wa kimataifa katika Umoja wa Mataifa wakati uongozi wa Afrika  haujumuishi kwenye meza za mazungumzo.”

Rais Mutharika ametaka ahadi mpya ya kuhakikisha kuna uwajibikaji wa pamoja na Afrika na Baraza hilo Kuu lisikilize sauti za Afrika.