Si hiyari, ni lazima kulikabili jinamizi la mabadiliko ya tabia nchi:Guterres

25 Septemba 2018

Mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 73 umefunguliwa rasmi hii leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. Wawakilishi kutoka nchi 193 wanachama, mashirika ya kimataifa, asasi za kiraia na wadau wengine wa maendeleo wakikutana kwa lengo la kuhakikisha ajenda ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa inatimia ifikapo 2030. 

 

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 73 akiwakaribisha wajumbe katika mjadala huo wa wazi. Na kisha kumwachia ukumbi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres  kutoa hotuba ya ufunguz.i

Katibu Mkuu Guterres hakutafuna maneno akianza kwa kutamka wazi kwamba imani imeota mbawa na kuiathiri vibaya dunia, kuanzia kwenye taasisi za kitaifa, miongoni mwa mataifa na hata katika masuala ya sheria na utulivu duniani.  Watu wamepoteza matumaini na ni wajibu wa kila mmoja kuyarejesha matumaini hayo.

’Leo hii dunia utulivu wa dunia unazidi kuparaganyika, mahusiano ya kiutawala hayaeleweki, maadhili ya dunia yameporomoka na misingi ya demokrasia ikibinywa. Na utawala wa sheria unakandamizwa khuku ukwepaji sheria ukiongezeka, kama viongozi na nchi lazima tuhakikishe kuna mipaka nyumbani na kwenye uwanja wa kimataifa. ‘’

Guterres amegusia mada mbalimbali akiwakumbusha nchi wanachama wanawajibika kimataifa kuyatekeleza ikiwemo suala la wakimbizi na wahamiji, kupambana na ugaidi, haki za binadamu, usawa na kutokomeza silaha za nyukilia lakini msisitozo akauweka kwenye masuala mawili mosi vita dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi

Tumefikia pabaya na tusipobadili muelekeo katika miaka miwili ijayo mabadiliko haya yatatupiga chenga na kufanya mambo kuwa mabaya zaidi sisi viongozi hatufanyi juhudi za kutosha, ni lazima tuwasilkilize wanasayansi, ni lazima tuone kinachotokea mbele ya macho yetu, tunahitaji malengo makubwa na hatua za haraka, lazima tuhakikishe utekelezaji wa mkataba wa Paris. Mustakbali wetu uko njia panda hakuna kilicho na kinga na mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri kila kitu”

Na pili ni hatari mpya zihusiananzo na maendeleo ya teknolojia ambayo amesema pamoja na kusaidia kuponya magonjwa, kukuza uchumi, kuunganisha biashara na jamii kote duniani lakini ina hatari kubwa

“Maendeleo ya teknolojia yanaweza kuathiri soko la ajira ambapo kazi ya jadi zinabadilika au kutoweka na idadi ya vijana wanaosaka ajira kuendelea kuongezeka, hivyo mafunzo yatahitajika kuliko ilivyotarajiwa awali, elimu lazima iende sanjari na teknlojia hiyo tangu madarasa ya awali. Serikali zitahitaji kufikiria mipango kabambe ikiwemo kuhakikisha kipato cha kawaida.”

Ameongeza kuwa yote haya yatawezekana tu kwa mshikamano wa kimataifa na kuwahimiza viongozi kwamba “Ni lazima turejeshe imani, mshikamano na utu kwa wote.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter