Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen iko taaban, bila hatua madhubuti itakuwa janga kubwa:Lowcock

Mtoto akisubiri mjini Hudaydah yemen wakati UNICEF ikigawa msaada wa nchini Yemen June 2018
UNICEF
Mtoto akisubiri mjini Hudaydah yemen wakati UNICEF ikigawa msaada wa nchini Yemen June 2018

Yemen iko taaban, bila hatua madhubuti itakuwa janga kubwa:Lowcock

Msaada wa Kibinadamu

Robotatu ya watu wa Yemen wanahitaji aina fulani ya msaada ili kuweza kusihi wakati mgogoro wa nchi hiyo ukiwa umeingia mwaka nne sasa.

Akizungumza katika mkutano maalumu kwenye kikao cha 73 cha Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani hii leo, Mkuu wa masuala ya kibinadamu na shirika la kuratibu misaada ya dharura la Umoja wa Mataifa , OCHA Bwana. Mark Lowcock amesema mgogoro wa Yemen ni janga lililowaathiri zaidi ya watu milioni 22, ambao hivi sasa wanahitaji msaada wa kibinadamu.

Watu wengine milioni 8.4 amesema wakikabiliwa na kutokuwa na uhakika wa chakula na milioni 10 wengine wakiwa katika hatihati ya kutumbukia katika hali hiyo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu endapo hatua madhubuti hazitochukuliwa.

Mark lowcock , Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura, akihutubia baraza la usalama kuhusu hali ya yemen.
Picha na UN/ Mark Garten
Mark lowcock , Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura, akihutubia baraza la usalama kuhusu hali ya yemen.

Katika mkutano huo wa ngazi ya juu uliojikita kwenye hatua za kibinadamu zinazochukuliwa kuwapunguzia madhila watu wa Yemen, mafanikio yaliyofikiwa na changamoto za kila siku katika kutafuta uungwaji mkono zaidi wa kimataifa Lowcock amesisitiza kuwa.

(SAUTI YA MARK LOWCOCK)

“Mgogoro wa kibinadamu nchini Yemen ndio mgogoro mbaya zaidi duniani, lakini pia ndio uliouvutia idadi kubwa na moja ya usaidizi mkubwa zaidi wa kibinadamu ulio na tija duniani.”

Ameongeza kuwa nusu milioni ya watu nchini Yemen wamelazimika kufungasha virago na kukimbia Hudaudah, milioni mbili ni wakimbizi wa ndani, kana kwamba adha hiyo haitoshi kipindupindu na magonjwa ya kuhara yamewaathiri watu zaidi ya milioni moja tangu April 2017.

Akifafanua zaidi kuhusu zahma hiyo ya kibinadamu kwa watu wa Yemen, Bi. Lise Grande mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini Yemen kwenye mkutano huo amesema

(SAUTI YA LIZ GRANDE)

“Hakuna nchi yoyote duniani ambayo idadi kubwa ya watu wake wanahitaji msaada ili kuishi kama Yemen, idadi inatisha na mwenendo unazidi kubwa mbaya, asilimia 80 ya watoto wote ambayo ni watoto milioni 11 wanahitaji msaada, na takriban mtoto mmoja hufa kila baada ya dakika 10 kwa sababu zinazotokana na vita.”

Hospitali nyingi nchini Yemen zimezidiwa uwezo. Hapa ni hospitali ya Al Thawra, Hodeidah nchini Yemen. 15 Aprili 2017
OCHA/Giles Clarke
Hospitali nyingi nchini Yemen zimezidiwa uwezo. Hapa ni hospitali ya Al Thawra, Hodeidah nchini Yemen. 15 Aprili 2017

Ameongeza kuwa si hayo tu lakini pia

(SAUTI YA LIZ GRANDE)

“Tunakadiria kuwa watoto elfu 10 wamepoteza maisha kwa sababu za mgogoro wa kibinadamu , asilimia 50 ya watoto wote Yemen wamedumaa, asilimia 70 ya wasicha hivi sasa wameolewa kabla ya kutimiza miaka 18 na tunafahamu tukiwa na hofu kubwa kwamba kuna visa zaidi ya 2600 vya watoto kuingizwa jeshini.”

Kwa mujibu wa OCHA wakati maelfu ya familia yakisalia bila chanzo chochote cha kipato wakiwemo waalimu, wahudumu wa afya, wafanyakazi wa sekta ya maji na usafi na watumishi wengine wa umma, wafanyakazi hao wa umma hawajalipwa mishahara yao kwa miaka miwli sasa.

Hivi sasa kuna mashirika ya misaada zaidi ya 150 nchini Yemen yakiwemo ya Umoja wa Mataifa ambayo yanafanya kazi usiku na mchana ili kutoa msaada wa chakula, malazi, lishe, ulinzi na zaidi kwa mamilioni ya raia wa Yemen ambao maisha yao yamesambaratishwa na vita vilivyoshika kasi 2015.

OCHA inasema dola bilioni 3 zinahitajika kwa ajili ya mipango ya usaidizi kwa mwaka huu, na habari Njema ni kwamba asilimia 65 sawa na dola bilioni 2 ya fedha hizo zimepatikana na kufanya ombi la msaada kwa Yemen kuwa moja ya maombi yaliyofadhiliwa kwa kiasi kikubwa zaidi duniani.