Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutumie busara za Mandela kukabili changamoto za sasa- Guterres

Sanamu ya shaba ya Nelson Mandela ikiwa na mikono iliyoinuliwa imesimama karibu na Maria Fernanda Espinosa Garces na Katibu Mkuu UN Antonio Guterres katika sherehe ya uzinduzi.
UN/Cia Pak Muonekano wa sanamu ya hayati mzee Nelson Mandela iliyozinduliwa leo kwenye makao makuu ya UN jijini New York, Marekani

Tutumie busara za Mandela kukabili changamoto za sasa- Guterres

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa leo umepitisha azimio la kumuenzi Nelson Mandela kutokana na mchango wake katika kusongesha  utu, amani na  haki za binadamu siyo tu nchini mwake bali duniani kote kwa ujumla. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

Tukio la kumuenzi Mzee Mandela lilianza kwa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa kukabidhi sanamu ya mzee Mandela kwa Umoja wa Mataifa.

Kisha hatua muhimu ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa  Mataifa ya kupitisha azimio la kumuenzi Mzee Mandela likiangazia mchango wake wa kutetea haki za msingi za binadamu, amani na kutatua migogoro yote iliyopo duniani kwa kutumia njia za amani.

Rais wa Baraza Kuu Maria Fernanda Espinosa akahoji na kutangaza kuwa azimio limepitishwa..

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na Katibu Mkuu UN António Guterres wakizindua sanamu ya shaba ya Nelson Mandela katika sherehe ya ndani.
UN/ Cia Pak Katibu Mkkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) na Rais wa Baraza Kuu María Fernanda Espinosa na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wakizindua sanamu ya hayati Mzee Nelson Mandela hii leo kwenye makao makuu ya UN, New York ,Marekani

Na ndipo Katibu Mkuu Antonio Guterres akahutubia hadhira hiyo iliyoleta pamoja viongozi wa nchi na wakuu wa serikali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akisema leo wanamkumbuka Mandela, mtu wa busara ya hali ya juu ambaye alisongesha masuala yaliyo msingi wa Umoja wa Mataifa , "Alithamini jamii iliyo huru na ya kidemokrasia ambamo kwayo watu waliishi  pamoja kwa usawa na amani. Alikabilia na watesi wake mahakamani, akitambua kuwa walikuwa na nguvu ya uhai na kifo chake na katu hakurudi nyuma.”

Na kama hiyo haitoshi, Guterres akasema kuwa "Na kila pahali, alikuwa bingwa wa amani, kusamehe, unyenyeku, upendo, utu na haki za binadamu."

Na  kwa mantiki hiyo Guterres amesema katika zama za sasa zenye tishio la haki za binadamu na amani Tunahitaji kukabiliana na mashinikizo haya kwa kutumia busara, ujasiri na uthabiti aliokuwa nao Mandela.”