Kwanini Brazil huwa ya kwanza kuhutubia UNGA?

24 Septemba 2018

Kawaida ni rais wa Brazil ndiye hufungua vikao vya ngazi za juu katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Lakini ni kwa nini? Utaratibu huu ulianza katika kikao cha mwanzo kabisa kilichofanyika mjini London, Uingereza Januari 10 mwaka 1946. Tangu wakati huo Brazil imekuwa kila mara inakuwa ya kwanza katika ratiba za viongozi kuhutubia mjadala wa wazi wa Baraza hilo unaofanyika kila mwezi Septemba.
 

Hamna mtu aliyechukua uamuzi kuwa Brazil ndiyo itakuwa ya kwanza katika orodha ya watakaozungumza katika vikao vya Baraza Kuu.Utaratibu wenyewe, ambao umekuwa ukiimarika kila mwaka, haukuwa na kanuni  yoyote bali ulitokea tu.

Frederico Meyer, mshauri mkuu wa zamani katika ubalozi wa kudumu wa Brazil katika Umoja wa Mataifa, aeleza, “Mataifa yaliyoshinda vita vikuu vya pili vya dunia hayakutaka kutawala  kikao cha kwanza cha Baraza Kuu, na enzi mpya ndiyo ilikuwa inaanza.

Ushirika mpya wa kimataifa wenye chagizo la demokrasia ambako wanachama wote walikuwa sawa ulikuwa ndio unazinduliwa na kila taifa lilikuwa na kura moja. Na nafasi ya  kuzungumza mwanzo katika Baraza hilo, ilipewa  mataifa ambayo hayakuwa miongoni mwa yale yaliyoibuka na ushindi katika vita vikuu vya pili vya dunia. Kwa hivyo Brazil ikashika nafasi ya kwanza katika orodha ya  mataifa yatakayo zungumza.”

Na  Brazil haitaki utaratibu huu kubadilishwa. Kwao ni jambo muhimu sana, na wanaamini kama suala  lenye umuhimu  kitaifa.

Brazil ilikuwa imewakilishwa na mwanabalozi aliyeheshimika, Balozi Luis Martins de Souza Dantas, ambaye alikuwa na uelewa mzuri wa masuala ya kimataifa. Mwanzo mwa karne ya 21, alikuwa  waziri wa mashauri ya kigeni wa Brazil kwa mihula miwili na katika kipindi cha miaka ya 1920 aliiwakilisha nchi yake, mara mbili, katika Baraza la Kuu Umoja wa Mataifa la wakati huo likijulikana kama ushirika wa kimataifa - yaani League of Nations- lililoanza mwaka wa 1919 hadi 1946.”

Hata hivyo kuna maelezo mengine ya jinsi ilivyotokea:

Vadim Perfilyev, Mkurugenzi wa zamani wa  idara ya Sekreterieti ya Umoja wa Mataifa, aliyefanya kazi hiyo kwa muda mrefu, akihusika na kutayarisha orodha ya wazungumzaji katika Baraza Kuu anasema "Ninavyojua mimi hakuna aliyejitolea kuanza kuzungumza mwanzo na Brazil ndiyo taifa pekee lililokubali kutangulia.

“Kinyume na sasa, lakini wakati ule hakuna aliyekuwa anataka kutangulia, wakidhani kuwa lingekuwa jambo jema kuzungumza baadaye. Mbali na hayo mkutano ulikuwa unafanyika kwa wiki nne”.

Hata hivyo kigezo kiliwekwa.

Frederico Mayer anaongeza kuwa, “mwaka uliofuata katika mkesha wa kikao cha pili cha Baraza Kuu, tulipokea taarifa  kutoka  sekreterieti ya Umoja wa Mataifa ikiuliza ikiwa Brazil ingetaka tena  kuanza,  na tukakubali. Tangu wakati huo, kila mwaka,  tumekuwa tukipokea barua kutoka Umoja wa Mataifa."

Je utaratibu huu umewahi kuzusha hoja?

Akijibu swali hilo, Vadim Perfiliev, anasema kuwa hilo halijawahi kutokea. Na  Brazil haitaki utaratibu huu kubadilishwa. Kwao ni jambo muhimu sana, na wanaamini kama suala  lenye umuhimu  kitaifa.

Kwa miongo, marais wa Brazil, mawaziri au mabalozi ndio huanza kuongea katika mijadala ya Baraza Kuu.
Na je Umoja wa Mataifa umekuwa ukifuata utaratibu huu. Frederico Meyer, akitabasamu anajibu “ndiyo na hapana.” 

 Utaratibu huo ulibadilishwa  kwa rais wa Marekani, wakati huo akiwa Ronald Reagan katika mwaka walipojaribu kumuua.Kikosi cha siri cha Marekani, kikihofia usalama wake, kilimleta Umoja wa Mataifa asubuhi, kutoa hotuba, na baada tu ya kukamilisha hotuba yake wakampeleka. Lakini katika mpangilio wa ratiba za siku, hotuba yake ilipangwa vingine, ikionyesha kama Brazil ndiyo ingeanza.

Mwanadiplomasia wa Brazil, ameeleza kuwa wanaamini kuwa  taarifa yao hutoa mwongozo wa mjadala mzima na kwa hivyo hotuba yenyewe kawaida huwa ni taarifa iliyotayarishwa na wakizungumza huwa ndiyo dunia nzima inawasikiliza wao.

Ameongeza kuwa kawaida katika kikao cha kwanza ukumbi huwa umejaa pomoni jambo ambalo ni kinyume na vikao vinavyofuata.
 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud