Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mnaopigana Tripoli heshimuni mkataba wa kusitisha mapigano: Guterres.

Askari wawili wa vikosi vilivyoko mjini Tripoli wakipita katika barabara za mji wa Bin Jawad karibu na bandari ya mafuta ya Sindra.
Photo: Tom Westcott/IRIN
Askari wawili wa vikosi vilivyoko mjini Tripoli wakipita katika barabara za mji wa Bin Jawad karibu na bandari ya mafuta ya Sindra.

Mnaopigana Tripoli heshimuni mkataba wa kusitisha mapigano: Guterres.

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ana wasiwasi kutokana na ongezeko la visa vya ukiukwaji wa mapatano ya kusitishwa  mapigano yaliyofikiwa tarehe 4 mwezi huu wa Septemba chini ya usimamizi wa mwakilishi wake maalum nchini humo Ghassan Salame.

 

Katika taarifa iliyotolewa mjini New York Marekani na msemaji wake, Bw. Guterres amezihimiza pande zote husika katika mgogoro huo kuheshimu mkataba huo na kujizuia  dhidi ya vitendo ambavyo vinaweza kuongeza mateso kwa raia wa kawaida.

Tamko hili la Katibu Mkuu linafuatia taarifa zinazosema kuwa mjini Tripoli pande kinzani zinapambana na kurusha makombora yaliyosababisha vifo vya jumla ya watu 106 na majeruhi 518 tangu tarehe 27 Agostu hadi jana Ijumaa.

Katibu Mkuu amekariri kuwa yeyote  aliyehusika na ukiukwaji wa  sheria za kimataifa za msaada wa kibinadamu  na pia sheria za kimataifa za haki za kibinadamu lazima awajibishwe.

Ametuma salamu za rambirambi kwa waliopoteza ndugu na jamaa zao na kuwatakia ahueni ya haraka majeruhi wa zahma hiyo.