Tuna wasiwasi na mayatima wa Ebola DRC:UNICEF

21 Septemba 2018

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia watoto, UNICEF likishirikiana   na washirika wao linasema limeorodhesha  watoto 155 ambao wamepoteza wazazi wao au waliachwabila mlezi kutokana na  mlipuko ugonjwa wa Ebola  uliotokea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Katika taarifa iliyotolewa leo na shirika hilo huko Kinshasa, nchini DRC, Dakar, Senegal, Geneva Uswisi na New York Marekani, UNICEF inasema kuwa idadi hii inawajumulisha watoto ambao wamepoteza mzazi moja au wawili ama wanaowatunza  ambao walifariki dunia kutokana na Ebola pamoja na wale amabo waliachwa bila mlezi baada ya wazazi wao kutengwa na kuwekwa katika vituo vya matibabu.

Taarifa inaendelea kuwa watoto ambao hupoteza wazazi wao kutokana na Ebola wanapata machungu mengi moyoni kwani hunyanyapaliwa, hutengwa na pia hushuhudia mzazi wake au mlezi wake akifariki dunia na hilo ndilo jambo linalowasumbua.

Kundi la watoto aina hiyo  liko hatarini na UNICEF ina wasiwasi na hali yao.

Mmoja wa watoto waliopoteza wazazi wao ana umri wa miaka 13 na katika jina alilopewa la Dieudonne ili kuficha utambulisho wake anasema alipoteza jamaa wanane,  “Wote walifariki dunia kutokana na Ebola.Ni familia yangu yote.Mwanzo alikuwa mama yangu ,kisha dada zangu na shangazi.Mwingine yuko Hospitali na nimewapoteza watu wanane wa karibu sana. Siwezi kujiua na ni lazima niendelee kuishi.”

 Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC, Dkt Gianfranco Rotigliano, anasema kumpoteza mzazi au mtu wa karibu inaweza kuwa hali ngumu kwa mtoto na jukumu lao kama UNICEF ni kuwalinda na vilevile  kusaidia watoto wote ambao wameathirika na virusi vya Ebola.

Wakati huo  huo, shirika la afya ulimwenguni WHO limetoa hali idadi ya waliofariki duniana ugonjwa wa Ebola nchini DRC.

Msemaji wa WHO, Bi.Fadela Chaib,akiwa mjini Geneva Uswisi leo Ijumaa amewambia wandishi habari kuwa hadi tarehe 18 mwezi huu idadi kamili ya visa vya Ebola vilivyoripotiwa ilikuwa 143, huku vilivyohakikishwa kuwa ndivyo112 na 31 ni shukiwa ilhali vifo ni 97.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter