Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yamkumbuka Annan, amwagiwa sifa lukuki

Mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la UN ulikutana kumkumbuka Kofi Annan
UN /Kim Haughton
Mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la UN ulikutana kumkumbuka Kofi Annan

UN yamkumbuka Annan, amwagiwa sifa lukuki

Masuala ya UM

Umoja wa Mataifa leo umekuwa na kumbukumbu maalum ya Katibu Mkuu wa 7 wa chombo hicho aliyefariki dunia mwezi uliopita akiwa na umri wa miaka 80.

Tukio hilo maalum limefanyika katika ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likileta viongozi mbalimbali wa Umoja huo akiwemo Katibu Mkuu wa sasa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa 8 Ban Ki-moon na familia ya Annan ikiongozwa na mkewe Nane Annan na watoto wao.

Akihutubia hadhira hiyo katika tukio lililotanguliwa na mpiga ngoma aliyetoa masifu ya mwendazake Annan, Bwana Guterres amesema kuwa Annan alisihi kila mtu asiwe mtazamaji katika maisha. Akisema kuwa “alitutaka sote tuchukue hatua dhidi ya upendeleo, ukatili na umwagaji damu. Alitetea ushirikiano wa kimataifa kwa kina, alikuwa muumini wa Umoja wa Mataifa na mfumo wa kimataifa ufuatao kanuni. Na lazima nisema, kifo chake kinauma sana kwa sababu hivi sasa tunahitaji zaidi kuliko wakati wowote imani hiyo.”

Naye Bwana Ban ambaye alipokea kijiti cha kuongoza Umoja wa Mataifa mwaka 2006 baada ya Kofi Annan kumaliza kipindi chake, amesema “nina uhakika kadri miaka inavyokwenda, historia itaonyesha kuwa  Kofi Annan alikuwa kiongozi wa kipekee. Hakuwa na majivuno lakini alizungumza na kusikilizwa. Alikuwa kiongozi aliyeshika mambo  ya zamani lakini alikuwa na dira thabiti ya kuangazia siku zijazo.”

Katibu Mkuu wa UN António Guterres (katikati) akiwa na Nane Annan, mke wa Kofi Annan (mwenye koti jeupe) pamoja na familia yake wakati wa kumbukumbu maalum ya Annan mjini New York, Marekani
UN /Mark Garten
Katibu Mkuu wa UN António Guterres (katikati) akiwa na Nane Annan, mke wa Kofi Annan (mwenye koti jeupe) pamoja na familia yake wakati wa kumbukumbu maalum ya Annan mjini New York, Marekani

Aliendelea kummwagia sifa akisema kuwa ni kiongozi ambaye ameacha dunia ikiomboleza kifo chake lakini pia ameipatia mchango wa kipekee ambao utakuwepo daima na utaendelea kuhamasisha.

Ndipo  ikawadia fursa ya Nane Annan, mke wa mwendazake Annan ambaye amesema, “amefariki dunia mapema mno akituacha tumevunjika moyo, lakini ameishi kadri alivyotaka, katika kipindi chote cha umri wa miaka 80. Mchango wake utaendelezwa kwenye taasisi yake na kwetu sote.”

Annan, mwanadiplomasia kutoka Ghana alichaguliwa kushika wadhifa huo kwa awamu mbili kuanzia mwaka 1997 hadi 2006.

Alisongesha mbele haki za binadamu na ulinzi wa amani duniani kote akipatia uhai zaidi Umoja wa Mataifa kwa kusisitiza uwepo wa Naibu Katibu Mkuu, ofisi thabiti ya maadili na kutokuvumilia kabisa ukatili wa kingono.

Wakati wa uongozi wa Annan kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Akiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa dunia walipitisha malengo ya milenia yaliyofikia ukomo mwaka 2015 na alishinda tuzo ya amani ya Nobel.

UN Video
Kofi Annan