Kuzama kwa MV Nyerere; Guterres aeleza mshikamano na Tanzania

21 Septemba 2018

Kivuko chazama nchini Tanzania na kusababisha vifo, Umoja wa Mataifa umetuma salamu za rambirambi ukisema uko tayari kusaidia kwa kadri itakavyohitajika kufanya hivyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea masikitiko yake kufuatia vifo  vilivyotokana na kuzama kwa kivuko kwenye ziwa Victoria nchini Tanzania siku ya Alhamisi.

Habari zinasema kivuko hicho MV Nyerere kilizama jana wakati kikiwa safarini kutoka eneo la Bugorora kisiwani Ukerewe kuelekea kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.

Vyombo hivyo vimeripoti kuwa hadi sasa takribani watu 100 wamethibitishwa kufa maji huku wengine wameokolewa wakiwa hai.

Katibu Mkuu ametuma salamu zake za rambirani kwa familia za waliopoteza  maisha pamoja na kwa serikali ya Tanzania huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Amesema Umoja wa Mataifa unashikamana na Tanzania wakati huu wa kipindi cha majonzi na uko tayari kusaidia kwa kadri itakavyohitajika.

Tayari Rais John Magufuli wa Tanzania ametangaza siku nne za maombolezo ya kitaifa ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud