Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kofi Annan kuenziwa na UN katika siku ya amani duniani hii leo

Kofi Annan (kulia)akiwa na msemaji wake, Fred Eckhard, wakiwa njiani kuelekea Angola kutoka Namibia.
UN Photo/Milton Grant
Kofi Annan (kulia)akiwa na msemaji wake, Fred Eckhard, wakiwa njiani kuelekea Angola kutoka Namibia.

Kofi Annan kuenziwa na UN katika siku ya amani duniani hii leo

Masuala ya UM

Umoja wa Mataifa leo utakuwa na tukio maalum la kumkumbuka Katibu wake mkuu wa 7 Kofi Annan aliyefariki dunia mwezi uliopita huko Uswisi na kuzikwa wiki iliyopita nyumbani kwake nchini Ghana.

Tukio hili maalum katika ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litaanza kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kugonga kengele ya amani ambayo ni zawadi kutoka Japan na baadaye tukio la kumuenzi Kofi Annan kwa mchango wake wa kusongesha amani na haki duniani.

Miongoni mwa watu wanaomkumbuka Kofi Annan ni aliyekuwa msaidizi wake maalum Corinne Mommal-Vanian ambaye akihojiwa hivi karibuni amesema amebaini siri ya Kofi kupendwa na kila mtu kwa kuwa alimuona akizungumza na wakimbizi na marais, na wasaidizi wake na wote alizungumza nao kwa njia moja.

“Kila mtu nadhani alikuwa wa kipekee kwake. Na unajua tulijadili ilikuwa jambo zuri katika zama hizi za mazingira magumu kuona watoto hawa wadogo wakimkimbilia wakiwa na tabasamu kwenye nyuso zao, unajua tena kuwa mtoto. Na hili ndilo lililomfurahisha hasa kuona  ubinadamu wa watu hawa ambao mara nyingi tunawaangalia kitakwimu, tukisema ‘hawa wakimbizi wa ndani’ au tunawachukulia katika mtazamo wa kisiasa wa Sudan na Baraza la Usalama.”

Tukio hili linafanyika leo likienda sambamba na siku ya kimataifa ya amani ambayo huadhimishwa tarehe 21 mwezi Septemba kila mwaka.

Katika ujumbe wake wa siku hii, Katibu Mkuu Guterres anakumbusha jamii ya kimataifa kuwa mwaka  huu ni wa kipekee kwa kuwa siku ya amani inafanyika wakati tamko la  haki za binadamu linatimiza miaka 70.

Amesema tamko hilo ni nyaraka ya msingi ambayo inakumbusha kuwa amani itaota mizizi na kushamiri katika jamii isiyo na njaa, umaskini au ubaguzi.

Bwana Guterres amesema kwa kuwa tayari kuna nyaraka hiyo adhimu, ni vyema kuhakikisha malengo ya maendeleo endelevu yanafanikiwa.

“Nawasihi mzungumze. Mzungumze kwa ajili ya usawa wa kijinsia. Kwa ajili ya jamii jumuishi. Kila hatua ina mchango wake,” amesema Katibu Mkuu akisema kuwa kila mtu atomize wajibu wake shuleni, kazini na nyumbani..

Kwa mantiki hiyo amesihi ushirikiano wa kila mtu ili kuendeleza na kutetea haki za binadamu kwa minajili ya kuwa na amani ya kudumu kwa faida ya wote.