Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Migogoro na hali ya hewa vyavuruga uwepo wa chakula katika mataifa mengi: FAO

Wananchi wa Uganda wakiendelea na shughuli za shamba.
UNDP Uganda/Luke McPake
Wananchi wa Uganda wakiendelea na shughuli za shamba.

Migogoro na hali ya hewa vyavuruga uwepo wa chakula katika mataifa mengi: FAO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO kuhusu hali ya chakula duniani inasema kuwa migogoro pamoja na mabadiliko ya tabianchi vinaendelea kuwa chanzo cha ukosefu wa uhakika wa chakula katika mataifa 39 duniani.

Ikipatiwa jina matarajio ya uzalishaji mazao na hali ya chakula duniani, ripoti inasema mataifa 31 kati ya hayo 39 yako Afrika ilhali 7 yako Asia na moja Karibea ambalo ni Haiti.

Ripoti hiyo ambayo imetolewa leo mjini Roma, Italia inasema mizozo isiyomalizika, matukio ya kupindukia ya hali ya hewa ikiwemo mafuriko na joto Kali vimesababisha nchi hizo kuendelea kuhitaji msaada wa chakula kutoka nje ikiwa ni kama ilivyo kuwa miezi mitatu iliyopita.

Kwa Afrika mataifa hayo ni pamoja na na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Nigeria, Kenya, Uganda na Sudan Kusini.

Mathalani kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, ripoti inasema mvua zisizotosheleza katika msimu wa kilimo zilipunguza mavuno huko Malawi na Zimbabwe

Nchini Malawi, ripoti inasema makadirio ya mavuno ya nafaka mwaka huu ni ya chini ya wastani ambapo idadi ya watu wasio na uhakika wa chakula inaweza kuwa mara mbili ya idadi ya mwaka jana na kufikia watu milioni 3.3.

FAO inasema makadirio ya uzalishaji nafaka kutoka nchi za kipato cha chini ambazo zinakabiliwa na ukosefu wa chakula  kwa mwaka huu ni tani milioni 490 ikiwa ni ongezeko kwa tani milioni19 tu zaidi ya wastani wa miaka mitano iliyopita.

Hata hivyo shirika hilo linasema kiwango hicho kidogo cha ongezeko ni ushahidi tosha kuwa pengo la kupungua kwa uzalishaji kutokana na matukio ya mabadiliko ya tabianchi huko kuisni mwa Afrika, Asia ya Kati na Yemen kunatabiriwa kuzibwa na ongezeko la  uzalishaji kwenye nchi za Mashariki ya mbali na Afrika Mashariki.