Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Benki ya Dunia yaishika mkono Bangladesh ili iboreshe huduma kwa warohingya

Watoto wa wakimbizi warohingya wakishiriki kwenye mtaalamu wa vijana au GEMS katika moja ya maeneo rafiki kwa wanawake huko kambini Cox's Bazar nchini Bangladesh
UNFPA Bangladesh/Allison Joyce
Watoto wa wakimbizi warohingya wakishiriki kwenye mtaalamu wa vijana au GEMS katika moja ya maeneo rafiki kwa wanawake huko kambini Cox's Bazar nchini Bangladesh

Benki ya Dunia yaishika mkono Bangladesh ili iboreshe huduma kwa warohingya

Wahamiaji na Wakimbizi

Benki ya Dunia imechukua hatua kusaidia Bangladesh kuimarisha huduma za afya  ili nchi hiyo iweze kukabiliana na mahitaji ya wakimbizi wa Rohingya waliosaka hifadhi eneo la Cox’s Baz ar nchini humo.

Hatua hiyo imefanikishwa leo huko Dhaka nchini Bangladesh baada ya pande mbili hizo kutiliana saini makubaliano ya kuipatia nchi hiyo mkopo nafuu wa dola milioni 50.

Fedha hizo ikiwa ni sehemu ya mradi wa kusaidia sekta ya afya itawezesha kutoa huduma ya afya, lishe kwa warohingya ikijumuisha huduma kwa wajawazito, watoto wachanga, afya ya barubaru, afya ya uzazi na kuwapatia usaidizi wahanga wa ukatili wa kijinsi hususan wanawake na wasichana kupitia vituo rafiki kwa wanawake.

Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Bangladesh Qimio Fan amesema wamechukua hatua hiyo kwa kuwa takribani warohingya milioni moja wanaishi kwenye kambi zilizojaa kupindukia wakikabiliwa na hatari ya milipuko ya magonjwa huku tayari wakikumbwa na viwango vya juu vya utapiamlo.

 

Wakimbizi  wa kabila la warohingya
WFP/Saikat Mojumder
Wakimbizi wa kabila la warohingya

 “Mkopo huu nafuu utasaidia serikali kupanga na kusimamia mipango yake ya afya, lishe na huduma za warohingya huku ikiendelea kutoa huduma hizo za wananchi wake,” amesema Fan.

Mradi huu wa kwanza ni sehemu ya miradi lukuki ambayo Benki ya Dunia imepanga kuelekeza Bangladesh ili iweze kuhimili wimbi la wakimbizi hao wa kabila la Rohingya ambao walianza kumiminika nchini humo tangu mwezi Agosti mwaka jana kutokana na mateso na mauaji yanayowakabili nyumbani kwao Myanmar.