Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen! Yemen! Yemen! Pande kinzani malizeni uhasama kwa faida ya raia- WFP

David Beasley,mkuu wa mpango wa chakula duniani, akizuru Sanaa, Yemen amabko mgorgoro mkubwa wa njaa umekuwa ukiendelea kwa mwaka sasa.
WFP/Marco Frattini
David Beasley,mkuu wa mpango wa chakula duniani, akizuru Sanaa, Yemen amabko mgorgoro mkubwa wa njaa umekuwa ukiendelea kwa mwaka sasa.

Yemen! Yemen! Yemen! Pande kinzani malizeni uhasama kwa faida ya raia- WFP

Amani na Usalama

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP David Beasley amezitaka pande zote zinazosigana nchini Yemen kumaliza mgogoro na kuunga mkono amani.

Kupitia taarifa aliyoitoa hii leo mjini Roma Italia, Bwana Beasley amesema linalomgusa zaidi ni watoto wasio na hatia, wanawake na wanaume wa Yemen na akasema kusitisha uhasama kutatoa nafasi kwa mashirika ya kibinadamu kutimiza hitaji lao la kusambaza chakula na huduma nyingine muhimu zinazohitajika kuokoa maisha Yemeni.

Amesema “kuwalenga watoa misaada au vifaa vya kusambazia misaada pamoja na miundombinu haipaswi kupewa nafasi Yemeni au kwingine kokote duniani. Na tumeshuhudia mashambulizi kwa wafanyakazi wetu, malori yetu, maghala yetu na hata tunakohifadhia nafaka zetu. Nina laani jaribio lolote la kutumia misaada ya kibinadamu kama mbinu za kufanikisha vita. Maghala ya WFP, magari, vifaa, tunapotunzia chakula na zaidi wafanyakazi wetu vyote havifungamani na upande wowote katika mgogoro huu.

Umoja wa Mataifa unasema watu milioni 18 nchini Yemen tayari wanakabiliwa na baa kubwa zaidi la njaa duniani ambapotheluthi mbili ya watu wote nchini humo hawafamu ni wapi watapata mlo ujao.

Msaada wa WFP umekuwa wa muhimu kuikinga nchi hiyo kuingia katika baa la njaa, lakini katika mazingira kama haya ambayo hatari na vikwazo vinazidi kuongezeka, inaelezwa kuwa kuna hatari ya kukwama.

 

Chakula kutoka mpangop wa chakula duniani FAO kikipakiwa katika meli kutoika Djibout hadi Yemen.
OCHA/Charlotte Cans
Chakula kutoka mpangop wa chakula duniani FAO kikipakiwa katika meli kutoika Djibout hadi Yemen.

 

Mwaka uliopita kila mwezi WFP iliwapatia chakula watu milioni 6 hadi 7 waliokuwa na njaa na shirika hilo linasema iwapo mgogoro utaendelea na kuharibu  zaidi hali ya uchumi, kuna uwezekano mkubwa uhaba wa chakula ukaongezeka kiasi cha kuongeza idadi ya watu wanaotegemea msaada wa chakula kuweza kuishi kuongezeka na kufikia watu milioni 12.

“Kutokana na nafasi ndogo, kupungua kwa usalama na uharibifu wa miundombinu unaoendelea, uwezo wetu wa kufikisha usaidizi kwa idadi hii ya watu itakuwa changamoto kubwa. Zaidi ni kuwa mahitaji ya misaada ya kibinadamu nchini Yemen yanaongezeka sambamba na kuongezeka kwa fedha zaidi, na kutokana na mahitaji ya misaada ya kibinadamu kuibuka duniani kote kote, suala la fedha kuhusu mgogoro huu linakuwa changamoto kubwa kwa jumuiya ya kimataifa” anaongeza Bwana Beasley.

Katika siku za hivi karibuni Yemeni imeshuhudia mapigano makali na kushuka kwa hali ya usalama kwneye mji wa bandara wa Hudaydah, mgogoro ambao umeongeza ugumu wa uchumi na kushuka kwa thamani ya fedha hali hiyo ikiathiri mamilioni ya wayemeni wasio na hatia.

 

Vijana wakicheza katika magofu shule moja mjini Sanaa Yemen, ambayo iliharibiwa katika mgogoro unaondelea nchini humo.
UN OCHA/GILES CLARKE
Vijana wakicheza katika magofu shule moja mjini Sanaa Yemen, ambayo iliharibiwa katika mgogoro unaondelea nchini humo.

 

Habari zinasema uchumi wa Yemeni umezidi kushuka katika wiki hizi za hivi karibuni hali hiyo ikiongeza maumivu katika kushuka kwa asilimia 180 ya thamani ya fedha ya Yemeni tangu ulipoanza mgogoro mwaka 2015. Gharama ya chakula cha kawaida imeongezeka kwa asilimia 32 katika miezi 12 hali hiyo ikiziacha familia zikishindwa kujipatia chakula.