Afrika tutaangazia amani na maendeleo endelevu - Balozi Modest Mero.

18 Septemba 2018

Mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unafunguliwa rasmi hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani. 

Mkutano huo unafunguliwa rasmi na Rais wa mkutano huo wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  María Fernanda Espinosa  kutoka Ecuador.

Ufunguzi rasmi wa leo unaashiria kuanza kwa mjadala wa ngazi ya juu wa mkutano huo wiki ijayo ukienda sambamba na mikutano ya ngazi ya juu ikiangazia masuala muhimu kama vile Kifua Kikuu na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa imezungumza na Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Modest Mero kuweza kufahamu ni masuala yapi ambayo Afrika itayapatia kipaumbele kwenye mkutano huu.

“Masuala ambayo ni ya kipaumbele kwa baraza hili la 73 la Umoja wa Mataifa yatakuwa ni amani na usalama katika dunia, kwa sababu migogoro imezidi kuwa mikubwa. Hata mataifa makubwa sasa yameanza kuingia kwenye migogoro kwasababu ya Korea Kaskazini. Kumekuwa na tatizo la nchi ambazo zinakuwa na hatua mbalimbali za kuzionea nchi nyingine kwa mfano kuna nchi kama za Belarusi, nchi za Kisovieti bado zina migogoro yake” anaeleza Balozi Mero.

Na kuhusu kile ambacho nchi za kiafrika zitapatia mkazo Balozi Modest Mero anaongeza…

“Cha msingi hasa kwa sisi waafrika tunataka sana kukazania sana suala zima la amani na la pili maendeleo endelevu kwa sababu bado nchi zetu zina umaskini mkubwa sana na katika kila sekta kuna maeneo mengi yanahitaji kufanya vizuri ili kuwafanya watu wetu waishi maisha ambayo ni bora zaidi”.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter