Mboni ya jicho kumwezesha mwanamke kupokea pesa zake- WFP

18 Septemba 2018

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa yamebuni mbinu mbadala za kuwasaidia wanawake wakimbizi wa Syria kupokea fedha zao za ujira moja kwa moja badala ya kupitishia kwenye akaunti za benki. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

Mashirika hayo lile la mpango wa chakula dunia, WFP na lile la masuala ya wanawake, UN-Women yamesema mbinu hiyo itasaidia wakimbizi wanawake wanaoshiriki kwenye mradi wa kulipwa ujira baada ya kufanya kazi unaondeshwa na UN-Women katika kambi za Za’atari na Azraq nchini Jordan.

Taarifa ya mashirika hayo iliyotolewa leo Roma, Italia na New York, Marekani imesema kwa  kawaida wakimbizi wanawake wataweka jicho lao kwenye kifaa maalum ambacho kitabainisha utambulisho wake na hivyo kuweza kupatiwa fedha zake.

Kupitia mbinu  hii mkimbizi badala ya kupokea pesa kupitia  benki, ataweza kuchukua moja kwa moja hata anapokuwa anafanya manunuzi kwenye maduka makubwa yaliyohusishwa kwenye mradi huo.

Hana Heraak mkimbizi katika kambi ya Za'atari anaangalia mashine ya kumulika mboni.(Picha:WFP/Shada Moghraby)

Halikadhalika, badala ya wanawake hao kupokea fedha zao katika tarehe maalum iliyopangwa, sasa wataweza kuchukua fedha hizo wakati wowote kwenye maduka hayo.

Hivi sasa wakimbizi wapatao 106,000 nchini Jordan wananufaika na mradi huu ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka, amesema mbinu hii ni muhimu kwa kuwa wanaelewa fika kuwa wakati wa migogoro wanawake wanapata mkwamo wa teknolojia na digitali wakilinganishwa na wanaume.

Amesema ni kwa mantiki hiyo UN-Women inashirikiana na WFP kubadili hali hiyo kwa kutumia teknolojia bunifu kuleta mageuzi kwa wanawake ambao wako katika mazingira magumu na pia kuchapuza juhudi za kuwawezesha kiuchumi wanawake kwa kiwango kikubwa.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud