Katika kila sekunde 5 mtoto 1 alifariki dunia mwaka 2017 kwa magonjwa yanayozuilika- UNICEF

18 Septemba 2018

Takribani watoto milioni 6.3 wenye umri wa chini ya miaka 15 walifariki dunia mwaka jana kutokana na magonjwa yanayozuilika, imesema ripoti mpya iliyotolewa na mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Mashirika hayo lile la kuhudumia watoto, UNICEF, la afya WHO, kitengo cha idadi ya watu cha Umoja wa Mataifa na Benki ya Dunia imesema kiwango hicho ni sawa na mtoto mmoja katika kila sekunde tano.

Ripoti inasema watoto milioni 5.4 kati ya hao waliofariki dunia, walipoteza maisha kaitika miaka mitano ya awali ya uhai wao ambapo nusu ya idadi hii ni watoto waliokuwa na umri wa chini ya mwaka mmoja.

Mark Hereward ni afisa kutoka UNICEF.

(Sauti ya Mark Hereward, afisa kutoka UNICEF)

“Chini ya umri wa miaka mitano bila shaka magonjwa yanakuwa na nafasi kubwa, na kabla hata ya kiwango kupungua, njia rahisi ya kukabiliana nayo ni chanjo na hii hupunguza idadi ya vifo. Na pindi unapofanikisha hilo, sababu inayofuatia ya vifo ni vichomi na kuhara, na yote yanaweza kutibika, lakini unahitaji mfumo wa afya na wahudumu wa afya ya jamii kushughulikia suala hili.”

Wazazi wakiwa na uhakika wa tiba na chanjo kwa watoto wao, nao pia wanaweza kushiriki kwenye shughuli za kujikwamua kiuchumi. Hapa ni Sierra Leone watoto wakipatiwa chanjo dhidi ya Polio.
UNICEF/Kate Holt
Wazazi wakiwa na uhakika wa tiba na chanjo kwa watoto wao, nao pia wanaweza kushiriki kwenye shughuli za kujikwamua kiuchumi. Hapa ni Sierra Leone watoto wakipatiwa chanjo dhidi ya Polio.

Hata hivyo ripoti imesema kikanda hatari ya mtoto mwenye umri wa kati ya miaka 5 hadi 14 kufariki dunia ni kubwa zaidi kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara kuliko Ulaya ambapo katika nchi hizo mtoto mmoja kati ya 13 atafariki dunia kabla ya kufikisha miaka 15.

Kwa nchi zenye kipato cha chini takwimu ni mtoto mmoja kati ya 185. Bwana Hereward akagusia pia tofauti kati ya nchi na nchi.

 (Sauti ya Mark Hereward, afisa kutoka UNICEF)

“Hapa kuna mambo mawili. Mosi ni kwamba wanawake walioelimika wapo katika familia zenye uwezo lakini la muhimu zaidi wana uwezo zaidi wa kubaini hatari za mtoto na hapa nisisitize anaweza kusema nataka kufanya huduma hii. Kwa hiyo siyo tu elimu ya mwanawake ambayo ni muhimmu bali ile taarifa ya kujisaidia ambayo mtu anahitaji bila kujali elimu yake, ili waweze kujitunza wao na pia watoto wao wakati wa kipindi muhimu cha uzazi.”

UNICEF imesema licha ya changamoto hizo idadi ya vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka imepungua duniani kote kutoka milioni 12.6 mwaka 1990 hadi milioni 5.4 mwaka jana.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter