UN yahaha kuwezesha kusafirisha nje ya nchi wagonjwa mahututi Yemen

17 Septemba 2018

Umoja wa Mataifa nchini Yemen uko kwenye harakati za kuwezesha kufunguliwa kwa safari za ndege ili kuwezesha wagonjwa mahututi kusafirishwa nje ya nchi kwa matibabu ya magonjwa ambayo hayawezi kutibiwa nchini humo.

 

Taarifa iliyotolewa mjini Sana’a Yemen na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA imemnukuu mwakilishi wa shirika la afya ulimwenguni nchini  humo WHO. Dkt. Nevio Zagaria, akitaja magonjwa hayo kuwa ni pamoja na saratani, magonjwa sugu na yale ya kasoro za viungo ambayo watu wamezaliwa nayo.

“Raia watakaonufaika na huduma hii ni wale wenye saratani ya damu, wenye uvimbe, saratani ya shingo ya kizazi na koo pamoja na wale wanaohitaji kupigwa mionzi na kubadilishiwa figo,” amesema Dkt. Zagaria.

Mapema Jumamosi iliyopita, mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini Yemen, Bi. Lise Grande, aliwasilisha nyaraka ya kwa mamlaka mjini Sana’a za kuwezesha kusafirisha wagonjwa mahututi kwa kutumia ndege za kukodi hadi maeneo ambako kuna huduma za kuwapatia matibabu sahihi.

WHO inashirikiana na pande zote kinzani kukubaliana kuhusu kanuni za kutumia njia hiyo ya anga ya kusafiri ambapo kampuni huru ya kimataifa imepatiwa kandarasi kukagua taarifa za wagonjwa ili kubaini kuwa wana uhalali wa kupata huduma hiyo.

Huduma hiyo ya kusafirisha wagonjwa mahututi kwenye nje ya nchi ya Yemen itatekelezwa kwa awamu ya kwanza ya miezi Sita.

Dkt. Zagaria amesema wanapongeza sana mpango huo na wale wote wanaosaidia akisema kuwa asilimia 80 ya wagonjwa watakaotumia ni wanawake na watoto ambapo mbinu hiyo ni tumaini lao la mwisho.

Watu milioni 22, sawa na asilimia 75 ya idadi ya watu wa Yemen, wanahitaji msaada wa kibinadamu.

Umoja wa Mataifa pamoja na washirika wake, kupitia ombi la pamoja la mwaka 2018 wanahitaji dola za bilioni 3 ili kuwasaidia mamilioni ya watu nchini Yemen.

Hadi sasa , taarifa ya OCHA inasema wamepokea dola milioni 1.92 ambazo ni sawa na asilimia 65 ya pesa zinazohitajika kutoa huduma nchini kote Yemen.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter