Kenya imepiga hatua kulinda watu wenye ulemavu wa ngozi- Ero

17 Septemba 2018

Nuru inaangazia nchini Kenye ambako nchi hiyo inaelekea kuwa bingwa wa kikanda katika kulinda watu wenye ulemavu wa ngozi samabmba na kuwapatia huduma za afya na elimu.

Kenya imepata mafanikio makubwa katika kuchukua hatua dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, amesema mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu wa ngozi Ikponwosa Ero.

Akizungumza mjini Nairobi Kenya hii leo mwishoni mwa ziara yake rasmi ya siku 10 nchini humo Bi. Ero ametaja mafanikio hayo kuwa ni katika huduma ya afya ingawa akisema bado hatua zaidi zinahitajika kuwezesha kundi hilo kupata haki.

Ametaja mafanikio ya Kenya kuwa ni pamoja na huduma za elimu na afya akisema kihistoria watu wenye ulemavu wa ngozi Kenya wamekuwa wakiachwa nyuma na kutumbukia kwenye mtego wa mashambulizi na hata kukosa usalama.

Hata hivyo amesema bado Kenya inapaswa kuchukua hatua zaidi kujengea uwezo wa kiuchumi na kijamii kundi hilo na familia zao ili waweze kujikwamua.

Bi. Ero ametaka ulinzi zaidi kwenye kaunti za Migori na Taita Taveta ambako amesema bado kuna hofu kubwa ya watu wenye ulemavu wa ngozi kushambuliwa.

“Ni muhimu kuendesha kampeni za kina nchini kote kuhamasisha umma hususan maeneo ya vijijini ili kuhakikisha mazingira yanayochochea mashambulizi yanashughulkiwa,” amesema Bi. Ero.

Pamoja na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanapatiwa vifaa vya usaidizi kama vile vya kuwezesha kuona, ili waweze kuimarisha mahudhurio shuleni, Bi. Ero amepongeza mpango wa serikali ya Kenya ya kushughulikia changamoto zilizopo.

Halikadhalika amesihi Kenya iandae mpango wa kina wa utekelezaji wa kitaifa wa kutokomeza ghasia dhidi ya watu wenye ulemavu, mpango ambao utaenda sambamba na ule wa kikanda uliopendekezwa na kamisheni ya haki za binadamu ya Muungano wa Afrika.

Mtaalamu huyo huru atawasilisah ripoti yake kamili ya ziara hiyo mbele ya Baraza la Haki za Binadamu mwezi Machi mwakani.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud