Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi dhidi ya walinda amani wa UN hayakubaliki- UNMISS

Walinda amani wa UN wakiwa katika doria huko juba Sudan Kusini.
UNMISS
Walinda amani wa UN wakiwa katika doria huko juba Sudan Kusini.

Mashambulizi dhidi ya walinda amani wa UN hayakubaliki- UNMISS

Amani na Usalama

Mlinda amani wa umoja wa mataifa anayehudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, UNMISS amejeruhiwa hii leo baada ya kupigwa risasi na askari wa jeshi la serikali nchini humo, SPLA.

Taarifa ya UNMISS iliyotolewa leo huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini,  imesema mlinda amani huyo kutoka Nepal alikuwa na wenzake kwenye msafara uliokuwa unatoka kambi yao ya Yei kuelekea kuteka maji majira ya saa mbili na nusu asubuhi ya leo.

Ni wakati wa msafara huo ambapo askari mmoja wa SPLA alianza kufyatua risasi hewani na pia kuelekea kwenye moja ya magari ya msafara na ndipo risasi ikamjeruhi mlinda amani huyo sehemu ya mguuni na askari huyo kutokomea kwenye umati wa watu.

UNMISS inasema walinda amani hao hawakuweza kujibu mashambulizi kwa kuepuka kujeruhiwa raia na tayari mlinda amani huyo amesafirishwa hadi Juba kwa matibabu zaidi.

Akizungumzia tukio hilo, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, David Shearer amesema  “mashambulizi haya ya moja kwa moja kwa walinda amani wa umoja wa mataifa ambao wako hapa kusaidia watu wa Sudani Kusini hayakubaliki. Serikali inapaswa kuwatafuta na kuwawajibisha walioyatekeleza haya.

UNMISS umeamua kuimarisha doria kwenye barabara ya Kaya hadi Yei ambayo hutumiwa na wakimbizi wanaorejea nyumbani. Picha: UNMISS

Bwana Shearer ambaye pia ni mkuu wa UNMISS amesema tukio la leo ni ushahidi wa “kukosekana kwa usimamizi na udhibti wa majeshi kulikosababisha kuwepo kwa askari wanaoendelea kukiuka haki za binadamu kwenye eneo hili. Ni wajibu wa serikali kudhibithi  majeshi yao.”

Mashambulizi haya ya leo asubuhi yanakuja baada ya kuwepo  ripoti za mapigano mapya kati ya serikali na vikosi vya upinzani katika eneo linalozunguka Kajo-Keji jimboni Equatoria ya kati.

Tayari mpango wa usitishaji mapigano (CTSAMM) umethibitisha kuwa unafuatilia kile kinachosemwa kuwa ni ukiukwaji wa makubaliano ya usitishaji mapigano katika eneo la Yei.

Kabla ya kumjeruhi mlinda amani huyo hii leo,  wanajeshi wa serikali walikuwa wamefyatua takribani risasi 50 kutoka umbali wa mita 500 ilipo kambi ya Umoja wa Mataifa saa 11 na dakika 20 alfajiri.

 “Utiaji saini wa makubalano mapya ya amani na pande zote zilizoko kwenye mgogoro siku tatu zilizopita kulionyesha matumaini ya siku zijazo. Inasikitisha kuwa pamoja na makubaliano mapya, mapigano yanaendelea katika eneo la jimbo la Equatoria ya kati”, amesema Bwana  Shearer.

Amehimiza kuwa makundi yote yanatakiwa kuacha mapigano kama makubaliano yanavyotaka na wasitishe vurugu na “pande zote zinatakiwa kufanya kazi pamoja kujenga kuaminiana kati yao na watu wa Sudani Kusini ambao wanateseka kutokana na mgogoro unaoendelea.