Viwango vya joto duniani ni vya juu tuchukue hatua zaidi kudhibiti- Guterres

Wito watolewa kulinda tabaka la ozoni.
UNEP
Wito watolewa kulinda tabaka la ozoni.

Viwango vya joto duniani ni vya juu tuchukue hatua zaidi kudhibiti- Guterres

Tabianchi na mazingira

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kuhifadhi tabaka la ozoni, Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres amesema mwaka huu umevunja rekodi ya joto kali duniani kote na pia kuwa ni wakati muhimu kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Kupitia ujumbe wake, Bwana Guterres amesema “wakati tunapolizungumzia tishio hili, tunaweza kuchukua hamasa kutoka azimio la Montreal, mfano mzuri wa namna dunia inaweza kuja pamoja kwa ajili ya watu na sayari.”

Aidha amesema wakati sayansi ilipoonyesha kuwa mambo mbalimbali ikiwemo gesi chafuzi zinazochochea kuharibu tabaka la ozoni, (CFCs) ambalo linalinda uhai wote duniani, dunia ilichukua hatua kwa malengo na muono wa mbali kwa kuzipiga marufuku.

“Shukrani kwa uwajibikaji wa dunia nzima, katikati mwa karne hii, tabaka la ozoni linatarajiwa kurejea katika hali yake kama ulivyokuwa mwaka 1980. Hata hivyo kazi hii haijakamilika”.

Bwana Guterres amesema makubaliano yaliyoafikiwa mjini Kigali Rwanda, ambayo yataanza kutekelezwa januari mosi mwaka 2019 yanaangalia zaidi  gesi kali za joto ambazo bado zinatumika katika mfumo wa kupooza au HFCs.

Mpaka sasa, nchi 46 zimepitisha makubaliano hayo ambapo Katibu Mkuu Antonio Guterres amezisihii nchi nyingine kufuata nyayo na kuonyesha uwajibikaji wao kwa ajili ya sayari yenye afya.

“Kwa zaidi ya miongo mitatu, makubaliano ya Montreal yamefanya mengi zaidi ya kuzuia tundu katika tabaka la ozoni; yametuonyesha namna ambavyo nchi zinaweza kuja pamoja kuzungumzia hatari wanayokabiliana nayo wote, ” Guterres amesema na kusisitiza, “ninahamasisha ari hiyo hususani uongozi bora wakati tunapambana kutekeleza mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kuhamasisha hatua tunazotakiwa kuchukua kwa haraka wakati huu”.