Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulizi kwenye ghala la chakula latishia uhai wa watu Yemen- WFP

Mhudumu wa afya akisajili watoto wagonjwa kwenye kijiji kimoja karibu na Hudaydah nchini Yemen. Vituo vingi vya afya nchini humo vimesambaratishwa na mapigano.
OCHA/Giles Clarke
Mhudumu wa afya akisajili watoto wagonjwa kwenye kijiji kimoja karibu na Hudaydah nchini Yemen. Vituo vingi vya afya nchini humo vimesambaratishwa na mapigano.

Shambulizi kwenye ghala la chakula latishia uhai wa watu Yemen- WFP

Msaada wa Kibinadamu

Mapigano katika mji wa bandari wa Hudaydah nchini Yemen ambayo yameharibu ghala la chakula la shirika la mpango wa chakula duniani, WFP yanatishia kudhoofisha jitihada za kulisha mamilioni ya watu katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita, amesema Herve Verhoosel msemaji wa WFP mjini Geneva Uswisi wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Bwana Verhoosel amesema mapigano yanayoendelea karibu na bohari ya chakula karibu na bahari  ya Shamu ambayo ni  muhimu kwa operesheni za WFP yanaweza kuathiri uwezo wa kuwalisha kwa mwezi mmoja watu milioni 3.5 wenye njaa kaskazini na katikati mwa Yemen.

Ameongeza kuwa kombora lililorushwa na kundi la wapiganaji ambalo halijafahamika, pia limepiga ghala la WFP jiji Hudaydah lililokuwa likitunza chakula cha kutosha kulisha watu 19,200 wenye mahitaji.

Kwa mujibu wa WFP, hali ya usalama Hudaydah inaporomoka kwa haraka na inatishia misaada ya kibinadamu kwa mji na viunga vyake ambako chakula ni haba.

Katika tukio jingine mwishoni mwa mwezi uliopita, lori la WFP lilipigwa bomu likiwa linasafirisha mzigo kwenda Al Tuhayta kusini mwa Hudaydah. Lori hilo hilo likiwa na maandishi ya wazi kabisa ya WFP lilikuwa limebeba takribani tani 30 za msaada wa chakula cha kutosha karibia watu elfu mbili kwa mwezi mmoja.

Image
Raia wa Yemen ambao wamekimbilia majimbo ya Taiz na Al-HudaydahPicha: © UNHCR/Shabia Mantoo

 

Hadi sasa washambuliaji wa lori hilo bado hawajatambuliwa na lilishambuliwa kilomita mbili kabla ya kufika lilikokuwa linaenda na dereva alijeruhiwa kwa kiasi kikubwa.

Vurugu zinazoendelea ni sehemu ya uonevu ulioanzishwa mwezi juni na muungano wa vikosi vinavyoiunga mkono serikali inayotambulika kimataifa ya Rais Abd Rabbuh Mansur Hadi.

Mapigano ya sasa yanaendeleza mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka mitatu kati ya vikosi vya serikali na vile vya wapinzani wa Houthi ambao wanaidhibiti bandari ya Hudaydah na mji mkuu, Sana’a.

Umoja wa mataifa unasisitiza kuwa bandari hiyo ni muhimu kwa juhudi za maisha ya kibinadamu nchini Yemen, kwa sababu kimsingi ni lango la chakula, nishati na dawa kuelekea  katika eneo linguine la nchi ambako wanalazimika kuagiza mahitaji ya kila siku.

“Pamoja na kudorora kwa hali ya usalama, shughuli za WFP zinaendelea, na tunafanya kila tunaloliweza kuhakikisha shughuli zinaendelea katika eneo lote bila kuingiliwa” anasema Bwana Verhoosel.

Amefafanua kuwa mwezi uliopita pamoja na mgogoro kuwa wa hali ya juu kusini mwa Hudaydah, WFP ilitoamsaada wa chakula kwa takribani watu laki saba kati ya watu laki tisa katika eneo ambalo linachukuliwa kuwa la hatari zaidi.