Heko viongozi Sudan Kusini kwa kutia saini mkataba ulioboreshwa- Guterres

13 Septemba 2018

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa António Guterres amesema kusainiwa kwa mkataba ulioboreshwa ili kutatua migogoro nchini Sudan Kusini (RARCSS) tarehe 12 mwezi huu wa Septemba 2018 ni maendeleo mazuri na muhimu.

Katibu Mkuu anazipongeza pande zote juu ya hatua hii na anapongeza jitihada za kikanda na kimataifa ambazo zimefanikisha kutia saini mkataba huo mjini Addis Ababa Ethiopia.

Kupitia taarifa iliyotolewa na naibu msemaji wa wake mjini New York Marekani hii leo, Katibu Mkuu anawataka waliotia saini mkataba huo kuutekeleza kikamilifu ili watu wa Sudan Kusini wapate hatimaye amani wanayostahili.

Amesema ni muhimu kwamba pande zote zisitishe uhasama kote Sudan Kusini.

Bwana Guterres amesema safari sasa bado ina changamoto kubwa na hivyo ni jukumu la jumuiya ya kimataifa kuendelea kufuatilia kwa ukaribu hali ya Sudan Kusini wakati wa utekelezaji wa RARCSS.

Amesema Umoja wa Mataifa unasimama kidete, kwa ushirikiano wa karibu na mamlaka ya ushirikiano baina ya kiserikali ya IGAD na Muungano wa Afrika kusaidia washiriki katika kutekeleza mkataba huo.

Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani wa Rais Riek Machar walitiliana saini mkataba huo mjini Addis Ababa baada ya miezi 15 ya mashauriano kufuatia kuvunjika kwa msururu wa mikataba ya kusitisha mapigano yaliyozuka nchini Sudan Kusini mwezi disemba mwaka 2013.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud