Mapigano Hudaidah yatishia mamia ya maelfu ya raia Hudaidah- OCHA

13 Septemba 2018

Maisha ya maelfu ya watu yako hatarini Hudaidah, amesema Bi Lise Grande, mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen.

Taarifa iliyotolewa leo mjini Sana’a Yemen na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibiandamu, OCHA imemnukuu Bi. Grande akisema kuwa "hali imedorora kwa kasi katika siku za hivi karibuni. Familia zina hofu kutokana na mabomu, na mashambulizi ya anga.”

"Watu wanajitahidi kuishi," amesema Bi Grande akiwa mjini Sana’a hii leo na kwamba "zaidi ya asilimia 25 ya watoto wana utapiamlo; watu 900,000 katika eneo hilo wanahitaji chakula na wajawazito 90,000 wako katika hatari kubwa. Familia zinahitaji kila kitu - chakula, fedha, huduma za afya, maji, usafi wa mazingira, vifaa vya dharura, msaada maalum na wengi wanahitaji makazi. Inahuzunisha kuona watu wengi wenye uhitaji mkubwa.”

Hudaidah ni kumbilio la mamilioni ya watu wanaotegemea msaada ambapo takribani asilimia 70 ya misaada yote ya kibinadamu na kila vyakula vya kibiashara kwa ajili ya kaskazini mwa Yemen inaingia kupitia bandari za Hudaidah na Saleef, kuelekea kaskazini mwa Hudaidah.

Kwa mujibu wa mratibu huyo vinu vya kuzalisha chakula mjini Hudaidah vinalisha mamilioni ya watu akisema “tuna wasiwasi hasa juu ya kinu cha Bahari ya Sham, ambacho sasa kina tani 45,000 za chakula, kutosha kulisha watu milioni 3.5 kwa mwezi. Ikiwa vinu vmeharibiwa au kuvurugwa, gharama za kibinadamu zitakuwa kubwa, "amesema Bi Grande.

Tangu katikati ya mwezi Juni mwaka huu mapigano yalipoanza, washirika wa misaada ya kibinadamu wametoa msaada wa dharura kwa watu 366,000 katika eneo la Hudaidah , watu 116,000 wamepokea misaada ya fedha na watu 152,000 wamefaidika kutokana na vifaa vya dharura na makazi.

Katika siku nne za utulivu mapema mwezi Agosti, waliwachanja watu 380,000 dhidi ya kipindupindu. Mwezi uliopita, washirika walisambaza msaada wa chakula kwa watu 700,000 katika jimbo.

Bi Grande, "wahusika katika vita vinavyoendelea wanalazimika kufanya kila kitu kinachowezekana kulinda raia na miundombinu ya kiraia na kuhakikisha watu wanapata msaada ambao wana haki nao na wanahitaji kuishi.

Yemeni ni eneo la mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani. Watu milioni ishirini na mbili sawa na asilimia 75 ya wakazi wote, wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi, ikiwa ni pamoja na milioni 8.4 ambao hawajui wapi mlo wao ujao utatoka.

Umoja wa Mataifa na washirika wake wanaomba dola bilioni 3 kupitia mpango wa dharura wa 2018 ili kusaidia mamilioni ya watu wenye uhitaji kote nchini. Hadi sasa, dola za Kimarekani bilioni 1.92, asilimia 65 ya rasilimali zinazohitajika, zimepokelewa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

Chanjo yaendelea Yemen huku mitutu ya bunduki ikimiminwa

Licha ya makombora kuendelea kuporomoshwa huko Hudaidah kusini magharibi mwa Yemen kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo wa kihouthi, mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la afya WHO, la kuhudumia watoto UNICEF na la kuhudumia wakimbizi UNHCR, yanaendelea na kampeni ya chanjo dhidi ya mlipuko wa kipindupindu.

Afya ya wakazi Yemen inategemea bandari ya Hudaidah -WHO

Kuendelea kwa mapigano mjini Hudaidah nchini Yemen kunahatarisha wakazi ambao ni waathirika wa moja kwa moja na asilimia 70 ya watu wanaotegemea huduma muhimu ikiwemo, huduma ya afya inayopita bandari iliyomo mjini humo.