Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNSOM yapata kiongozi mpya

Nicholas Haysomm aliyekuwa mwakilishi maalum  Katibu Mkuu wa UN kuhusu Somalia.
Photo: UN Photo/Rick Bajornas
Nicholas Haysomm aliyekuwa mwakilishi maalum Katibu Mkuu wa UN kuhusu Somalia.

UNSOM yapata kiongozi mpya

Masuala ya UM

Nicholas Haysom, raia wa Afrika Kusini ameteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuwa mwakilishi wake nchini Somalia.

Anachukua nafasi inayoachwa na Michael Keating anayemaliza muda wake mwisho wa mwezi huu, na ambaye Bwana Guterres amempongeza kwa kazi yake nzuri na  uongozi bora.

Uteuzi wa Bwana Haysom ambaye pia ataongoza ofisi ya Umoja wa Mataifa ya  usaidizi kwa Somalia,UNSOM umetangazwa leo jijini New York, Marekani kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Bwana Haysom ambaye kitaaluma ni mwanasheria anaanza kazi yake mpya rasmi  tarehe mosi mwezi ujao na hivi sasa ni mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Sudan na Sudan Kusini,  kazi ambayo amefanya tangu  mwaka wa 2016.

Ameshika nyadhifa zingine mbalimbali ikiwemo Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Afghanistan kuanzia mwaka 2014 hadi 2016.

Mbali na nyadhifa mbalimbali katika Umoja wa Mataifa lakini pia ametumikia serikali ya Afrika Kusini kama mshauri mkuu wa masuala ya kisheria katika ofisi ya rais kuanzia mwaka wa 1994 hadi 1999.

Ana shahada katika sheria kutoka Vyuo Kikuu vya Natal na Cape Town nchini Afrika Kusini.