Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bayonuai ni kila kitu tufanye kila njia tuihifadhi- Dkt. Palmer

Vimbunga vya kila mara vimeharibu  mimema na kuua mifugo nchini Bangladesh
©FAO/Munir Uz Zaman
Vimbunga vya kila mara vimeharibu mimema na kuua mifugo nchini Bangladesh

Bayonuai ni kila kitu tufanye kila njia tuihifadhi- Dkt. Palmer

Tabianchi na mazingira

Katibu Mtendaji wa mkataba wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa tofauti za kibiolojia, Dkt. Cristiana Paşca Palmer amezungumzia umuhimu wa mkutano wa kimataifa kuhusu bayonuai utakaofanyika mwezi Novemba mwaka huu huko Sharm el-Sheikh nchini Misri.

Akihojiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira UNEP Dkt. Palmer amesema mkutano huo ni muhimu kwa kuzingatia umuhimu wa bayonuai  kwa maisha duniani.

“Bayonuai ni msingi wa chakula, dawa, mafuta na maisha. Ni chanzo cha utajiri wetu wa kitamaduni na kiroho. Kwa kuhifadhi, kurejesha na kutumia bayonuai kwa uendelevu, tunahakikisha kuwa tuna ufumbuzi wenye ufanisi wa changamoto zilizopo na za baadaye, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa, uhaba wa maji, usalama wa chakula, maendeleo endelevu, na amani na usalama” amesema Dkt. Palmer.

Kwa kuwa mazingira asili na bayonuai hivi sasa viko katika hali mbaya, Dkt. Palmer anasema ni muhimu nchi zivuke vikwazo vifuatavyo ili kukabiliana na hali hiyo.

Kwanza, “mfumo wa sasa wa uchumi duniani na muundo wa maendeleo hautilii maanani mtaji wa kiasili na mifumo ya kiasili itokanayo na mazingira ya kibayonuai. Tunapaswa kuondokana na mfumo wa kiuchumi unaofanya kazi katika mazingira yaliyojifunga yaani sawa na mipaka ya kisayari.”

Pili ametaja  kikwazo kitokanacho na mipango ya muda mfupi ya kisiasa akisema kuwa mipango mingi ya kimazingira na  uhifadhi ni ya muda mrefu kwa hiyo ni lazima mipango hiyo ya kisiasa iendane na ile ya kimazingira.

Na kikwazo cha tatu alichokitaja akisema ni kikubwa na  ni dhana kuu ya kujitenga kwa binadamu na asili ambapo Dkt. Palmer amesema mabadiliko makubwa yanatakiwa katika fikra za wanaotoa maamuzi, wazalishaji na walaji.

Katika mkutano  huo wa Sharm el-Sheikh wajumbe watajadili vitendo vinavyohitajika kuimarishwa ili kulinda viumbe hai ambavyo vinasaidia maendeleo endelevu na maisha duniani.

Halikadhalika watakubaliana juu ya sura ya majadiliano ya mwaka 2020, katika mpango mpya wa kimataifa wa Asili - mfumo wa baada ya mwaka 2020 kwa viumbe hai.