Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde tusaidieni vifaa vya ulinzi wa amani- Lacroix

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa, Jean-Pierre Lacroix akihutubia Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa. Picha: UM/Eskinder Debebe

Chonde chonde tusaidieni vifaa vya ulinzi wa amani- Lacroix

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umesema mkakati wake wa kuimarisha operesheni za ulinzi wa amani ulioanza kutekelezwa mwezi Machi mwaka huu umeanza kuzaa matunda.

 

Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana leo mahsususi kujadili marekebisho  ya ulinzi wa amani na utendaji wake, Mkuu wa operesheni hizo kwenye Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix ametolea mfano udhibiti ambao umewezesha kupungua kwa idadi ya vifo vya walinda amani.

Amesema kuanzia tarehe mosi Januari mwaka huu hadi tarehe 31 mwezi uliopita wa Agosti idadi ya walinda amani waliouawa katika mashambulizi ni 17, idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na 26 katika kipindi kama hicho mwaka jana. “Kiwango hiki ni pungufu kwa asilimia 32 lakini nataka tuwe na tahadhari kwa sababu vitisho dhidi ya walinda amani wetu bado vipo.”

Nataka kusisitiza kuwa kila mlinda amani mmoja anayeuwa ni sawa na walinda amani wengi. Tunaomboleza vifo vyao na tunakumbushwa kuwa lazima tuimarishe ulinzi na usalama wa walinda amani.

“Nataka kusisitiza kuwa kila mlinda amani mmoja anayeuwa ni sawa na walinda amani wengi. Tunaomboleza vifo vyao na tunakumbushwa kuwa lazima tuimarishe ulinzi na usalama wa walinda amani. Ni muhimu mtuwezeshe tuweze kutekeleza majukumu yetu kwenye nchi ambazo wanahudumia,” amesema Bwana Lacroix.

Ni kwa mantiki hiyo Mkuu huyo wa idara ya ulinzi wa amani ya Umoja wa Mataifa akatoa wito kwa nchi wanachama..

(Sauti ya Jean-Pierre Lacroix)

“Ningependa pia kuchukua fursa hii kutoa wito kwa nchi wanachama hususan zile zenye uwezo wa juu zaidi kijeshi zichangie zaidi polisi na wanajeshi kwenye ulinzi wa amani. Bado tuna mahitaji makubwa muhimu kama vile helikopta, vifaa vya kukabiliana na vilipuzi, vikosi vya kuchukua hatua haraka, kubaini hali ilivyo na usaidizi wa kimatibabu. Tunakaribisha  mchango katika maeneo hayo.”

Bwana Lacroix pia akagusia umuhimu wa kuwepo kwa wanawake wengi zaidi kwenye ulinzi wa amani akisema wanafanya ulinzi wa amani kuwa fanisi zaidi. Tunahitaji kuongeza idadi yao kwa walinda amani wanaotekeleza majukumu yao kiraia na pia kwenye sare za jeshi. Tunapaswa kuhakikisha kuwa wanaweza kushiriki vyema katika kazi yetu. Wanawake hivi sasa ni asilimia 21 tu ya watendaji wetu. Lazima tuchukue hatua zaidi, ” amesema mkuu huyo wa operesheni za ulinzi wa amani.

 

Sarah Blakemore Afisa Mtendaji Mkuu wa shirika la kiraia la Keeping Children Safe linalohusika na ulinzi wa watoto kwenye mizozo.
UN Photo/Loey Felipe
Sarah Blakemore Afisa Mtendaji Mkuu wa shirika la kiraia la Keeping Children Safe linalohusika na ulinzi wa watoto kwenye mizozo.

Wajumbe wa Baraza pia walimsikiliza Sarah Blakemore ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa shirika la kiraia la Keeping Children Safe linalohusika na ulinzi wa watoto kwenye mizozo. Bi. Blakemore ametaka uwepo wa mifumo thabiti ya kuepusha ukatili wa kingono na pale unapotokea basi wahanga walindwe na wasaidiwe na wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

 “Mara  nyingi wahanga hawana njia ya kuripoti ukatili, hawana matibabu au huduma ya kisaikolojia na hawajui la kufanya kusaka haki. Tunatoa wito kwa viongozi wa dunia wasongeshe usalama wa watotokwa kiwango cha juu kwa kutaka mashirika yanayohusika na ulinzi wa amani yatekeleze viwango vya kimataifa vya kulinda watoto ikiwemo kuwa na wachechemuzi wa haki za wahanga,” amesema Bi. Blakemore.