Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka uchuuzi wa karanga hadi kusafirisha China

Dizeli chafu zinachangia katika uharibifu wa hewa kupitia magari. Hapa ni  wachuuzi wakiuza bidhaa zao barabarani nchini Ghana
Jonathan Ernst/World Bank
Dizeli chafu zinachangia katika uharibifu wa hewa kupitia magari. Hapa ni wachuuzi wakiuza bidhaa zao barabarani nchini Ghana

Kutoka uchuuzi wa karanga hadi kusafirisha China

Ukuaji wa Kiuchumi

Jukwaa la kimataifa la kuchagiza biashara ya nje likikunja  jamvi hii leo huko Lusaka nchini Zambia, kijana mmoja mjasiriamali kutoka Gambia ameelezea jinsi ambayo ameweza kukuza biashara yake ya karanga  kutoka uchuuzi wa barabarani hadi kusafirisha nje ya nchi.

Mommar Taal muasisi wa kampuni ya Tropingo Food ya kuuza karanga na maembe yaliyokaushwa amemweleza Stella Vuzo wa Umoja wa Mataifa anayehudhuria jukwaa hilo kuwa…

(Sauti ya Mommar Taal)

“Nilianza kwa kuuza gunia moja la karanga la kilo 50 na baada ya muda niliweza kuuza lori zima kwa wateja wangu na kujenga nao uhusiano mzuri ambao hatimaye walianza kuniongezea mtaji.”

Hata hivyo amesema baada ya kupata mafunzo ya kujiamini na uendeshaji wa biashara aliweza kufungua kampuni yenye wafanyakazi 280 ambapo asilimia 90 ni wanawake, na kuanza kununua kwa kiasi kikubwa karanga kutoka kwa wakulima na ambazo soko kubwa ni China.

(Sauti ya Mommar Taal)

Mahitaji ni makubwa zaidi China, halikadhalika mfumo wa biashara ni rahisi na hauna mkwamo kupeleka bidhaa China.”

Alipoulizwa kuhusu mtaji alipata wapi, Mommar amesema..

(Sauti ya Mommar Taal)

“Baada ya miaka michache nilitoa taarifa kuwa nataka kuingia kwenye biashara ya nje na kutumia akiba yangu kuanza kuuza kontena za karanga. Kiasi kikubwa cha fedha kilitokana na akiba yangu na pia msaada wa wateja wangu ambao hatimaye walifadhili bidhaa zangu.”

Mjasiriamali huyo kijana ametoa wito kwa serikali za Afrika kutekeleza kwa vitendo sera za mipaka huru ya biashara akisema kwa kiasi kikubwa ziko kinadharia lakini wanakabiliwa na changamoto kubwa wanaposafirisha bidhaa nje ya mipaka ya nchi zao.