Kafando ahitimisha ziara Burundi aelekea Dar es salaam
Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi Michel Kafando amehitimisha ziara yake ya wiki nzima nchini humo iliyomkutanisha na wawakilishi wa serikali, vyama vya siasa na mashirika ya kiraia ambapo amewachagiza washiriki kwenye awamu mpya ya mazungumzo ambayo yanatarajiwa kuitishwa mwishoni mwa mwezi huu yakisimamiwa na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Mwandishi wetu wa maziwa makuu Ramadhani KIBUGA ametutumia taarifa hii kutoka Bujumbura, Burundi.
Kulingana na taarifa ofisi ya Umoja wa mataifa hapa Burundi, Mjumbe huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Michel Kafando alikuwa na mazungumzo na Waziri wa mambo ya nje na kuangazia ushirikiano kati ya Burundi na Umoja wa mataifa pamoja na ushiriki wa serikali kwenye raundi mpya ya mazungumzo yanayosimamiwa na Jumuiya ya Afrika ya mashariki.
Kwenye ziara hiyo, Bwana Kafando alikuwa pia na vikao kwenye nyakati tofauti na wakuu wa chama tawala na washiriika wake wa karibu pamoja na wapinzani wakiongozwa Muungano wa Amizeri Y’ Abarundi.
Taarifa hiyo inasema walizungumza maendeleo ya kisiasa nchini Burundi , ikiwemo uitishwaji wa raundi ya tano ya mazungumzo . Kwa Mujibu wa Kafando , pande zote mbili zimethibitisha azma ya kushiriki kwenye mazungumzo hayo kukiwa na matumaini ya kufikia maelewano ya kumaliza mgogoro unaoikabili Burundi.
Mjumbe huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa alikutana pia na wawakilishi wa mashirika ya wanawake na kuzungumzia ushiriki wa wanawake sawa na mashirika ya kiraia kwenye raundi hiyo mpya ya mazungumzo.
Mwanadiplomasia huyo amejadiliana pia na wawakilishi wa jumuiya ya kimataifa wakiwemo katibu mkuu wa Kongamano la maziwa makuu CIRGL, mwakilishi wa Muungano wa afrika, mabalozi, pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa. Mbali na maswala kuhusu mazungumzo, wamezungumzia pia hali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Burundi.
Kwenye taarifa hiyo, Bwana Kafando amesema alikuwa na mazungumzo mazuri na ya kufana na wadau mbalimbali wa siasa za Burundi. Amewachagiza wanasiasa wote kushiriki vikao hivyo na kufikia makubaliano katika raundi hiyo ijayo ya mazungumzo . Pia ameomba Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuisapoti Burundi katika juhudi zake za maendeleo.
Mjumbe maalumu wa katibu Mkuu Michel Kafando ameondoka Bujumbura jumatano hii na kuelekea Dar Es Salaam Tanzania ambako atakuwa pia na mashauriano na msuluhishi katika mgogoro wa Burundi Benjamin Mkapa.