Skip to main content

Myanmar yatumia sheria kuziba midomo wana habari- Ripoti

Wakimbizi wa Rohingya
Photo: WFP/Saikat Mojumder
Wakimbizi wa Rohingya

Myanmar yatumia sheria kuziba midomo wana habari- Ripoti

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa kujieleza nchini Myanmar imesema sheria zisizofafanuliwa vizuri zinatumiwa kudhibiti uandishi huru wa habari  nchini kote ikiwemomajimbo ya Kachin, Shan na Rakhine.

Ripoti hiyo iliyotolewa hii leo huko Geneva, USwisi inasema kuwa hali hiyo imesababisha waandishi wa habari washindwe kufanya kazi zao bila uhuru na upendeleo.

Wakati hukumu ya wiki iliyopita dhidi ya wanahabari wawili wa shirika la habari la Reuters, Kyaw Soe Oo na Thet Oo Maung, ilikuwa mfano mzuri wa hali ya juu wa unyanyasaji wa mahakama dhidi ya vyombo vya habari nchini Myanmar, ripoti  hii inaelezea mifano mingine kadhaa ya kuwekwa ndani na mashtaka dhidi ya waandishi wa habari na vyanzo vyao, vitendo vinavyoonyesha mwelekeo mkubwa wa kukandamiza uhuru wa kujieleza.

Ripoti inataja sheria ya mawasiliano ya simu, siri rasmi za serikali, utumaji wa fedha kwa njia ya kielectroniki, kuagiza bidhaa na safari za anga kuwa mambo yanayotumiwa dhidi ya wanahabari katika kesi nyingi kwa miaka mingi.

Mathalani ripoti imetoa mfano wa kesi moja ambapo waandishi wa habari watatu walikuwa miongoni mwa watu saba waliokamatwa Juni 2017 kwa kuripoti tukio la kuadhimisha siku ya kimataifa dhidi ya matumizi na usafirishaji wa madawa ya kulevya katika eneo liloloko chini ya udhibiti wa wapiganaji wa Ta’ang National Liberation Army (TNLA) kaskazini mwa jimbo la Shan.

Ripoti imesema ingawa waandishi wa habari kutoka gazeti la ‘The Democratic Voice of Burma’ na ‘The Irrawady’ walikuwa wakiripoti tukio la kuteketeza madawa ya kulevya na haikuwa kuhusiana na mgogoro wa kijeshi, walishitakiwa chini ya Sheria ya ushirikiano haramu, ambayo hutumiwa mara kwa mara kuhusisha mawasiliano na makundi ya kikabila yenye silaha na kwamba ni kosa la jinai.

"Ukweli kwamba waandishi hao wa habari  walikuwa wakiripoti kuhusiana na shughuli iliyoandaliwa na TNLA na isiyohusiana na mgogoro wa kijeshi, ni ishara jinsi mamlaka zinavyoona kuwa waandishi wa habari wamevuka mipaka ya kile mamlaka inachokiona ni taarifa zinazokubalika na  zisizokubaliwa," ripoti inasema.

Mashtaka dhidi ya waandishi hao yalifutwa baada ya kuwa wamekaa korokoroni kwa siku 67.

Akigusia ripoti hiyo, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amesema ripoti hiyo imesisitiza hatari wanazokabiliana nazo waandishi huru wa habari nchini Myanmar.

"Mahali ambako waandishi wa habari wanafungwa kwa kutembelea eneo ambalo liko chini ya udhibiti wa kundi la wapiganaji, pale ambapo vyanzo vyao vya habari vinafungwa jela kwa kutoa taarifa kutokea katika maeneo yenye mgogoro, na ambapo kuandika tu chapisho katika Facebook kunaweza kusababisha mashtaka yanayohusishwa na uhalifu,  mazingira kama hayo hayafai kwa mabadiliko ya kidemokrasia ," amesema Bi. Bachelet.