Bachelet ahutubia kwa mara ya kwanza Baraza la Haki za binadamu

10 Septemba 2018

Kamishna Mkuu mpya wa haki za binadamu wa Umoja wa  Mataifa Michelle Bachelet amehutubia kwa mara ya kwanza kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo huko Geneva, Uswisi na kugusia mambo kadhaa ikiwemo ukiukwaji haki za binadamu dhidi ya warohingywa na huko Syria.

Michelle Bachelet ambaye amechukua wadhifa huo tarehe mosi mwezi huu wa Septemba amegusia suala la ukiukwaji wa haki za bindamu dhidi ya waislamu wa kabila la Rohingya nchini  Myanmar akipendekeza utaratibu wa kimataifa wa kukusanya ushahidi wa uhalifu ikiwemo mauaji na mateso dhidi ya kabila hilo.

 (Sauti ya Michelle Bachelet)

 “Ni lazima nisistize umuhimu wa haki kwa Mynamar, nakaribisha  hatua za mwanzo za mahakama ya makosa ya jinai ya kimataifa, ICC kuwa ina mamlaka ya kisheria juu ya madai ya kufukuzwa kwa warohingya kutoka Mynamar  na uwezekano wa kuwepo kwa makosa megine ya jinai. Hii ni hatua  muhimu kuelekea kukomesha watu kutochukuliwa hatua na pia kushughulikia suala la mateso ya waRohingya..”

 Amezungumzia pia mgogoro unaoendelea huko Idlib nchini Syria akisema kuwa ..

 (Sauti ya Michelle Bachelet)

 “Nina wasiwasi  na mgogoro unaonyemelea Idlib nchini Syria. Mateso ya watu wa Syria yamekuwa mabaya. Nayahimiza mataifa yote  kuchukua hatua zote zifaazo kuona kama yanahakikisha ulinzi wa raia na pia kusaka haki dhidi ya ukikwaji wa haki za binadamu ambavyo wamepitia.”

Bachelet, ambaye ni rais wa zamani wa Chile, pia amesema ana nia ya kutuma ujumbe  nchini Austria na Italia ili kutathmini ongezeko la ghasia  na ubaguzi  wa rangi vinavyoripotiwa kufanyika katika nchi hizo dhidi ya wahamiaji na kuona jinsi gani ya kulinda kundi hilo.

Halikadhalika ametoa onyo kuhusu visa vya chuki dhidi ya wahamiaji nchini Ujerumani vinavyooeneka kuchochewa na hotuba za chuki dhidi ya wageni.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud