Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna uwezekano mkubwa wa kutokea El Nino mwishoni mwa mwaka huu:WMO

Ukame  unazidi kuathiri ardhi ya sehemu kubwa katika  bara la Afrika.
UNICEF/Mukwazhi
Ukame unazidi kuathiri ardhi ya sehemu kubwa katika bara la Afrika.

Kuna uwezekano mkubwa wa kutokea El Nino mwishoni mwa mwaka huu:WMO

Tabianchi na mazingira

Mwishoni mwa waka huu wa 2018 kuna uwezekano mkubwa wa kuzuka matukio ya El Nino kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa leo na shirika la hali ya hewa duniani WMO.

 

Shirika hilo linasema uwezekano wa kuzuka kwa hali hiyo ni asilimia 70 na taarifa za mapema zitazisaidia jamii kujiandaa na matukio yanayoambatana na hali hiyo kama mvua kubwa, mafuriko na ukame.

Kwa mujibu wa katibu mkuu wa WMO Petteri Taalas, mabadiliko ya tabia nchi yanachangia kwa kiasi kikubwa kubadilisha mzunguko wa matukio ya El Nino na La Nina pamoja na athari zake katika jamii.

Kwa mfano amesema mwaka 2018 ulianza na hali dhaifu ya La Nina lakini hali hiyo haikutosheleza kupunguza mwenendo wa joto Kali lililotawala na hii ikimaanisha kwamba mwaka 2018 uko mbioni kuwa moja ya miaka yenye joto la kupindukiaduniani.

Mabadiliko hayo pia yamesababisha kuendelea kwa matukio mengine kama mafuriko makubwa Japan, India na Kusini mwa Asia, pia moto wa nyikani uliosababisha harasa kubwa Marekani ikiwemo kukatili maisha ya watu.

Hata hivyo WMO inasema haitarajii hali ya El Nino kuwa mbaya zaidi kama ilivyokuwa 2015-216 lakini bado italeta athari kubwa, ingawa shirika hilo linaamini utabiri huu wa mapema utasaidia kuokoa maisha na kupunguza athari za kiuchumi.

Hii ni mara ya kwanza WMO inajumuisha utabiri wa El Nino katika mtazamo wake wa kimataifa wa hali ya hewa kwa msimu wa Septemba hadi Novemba.