Tumesaidia nchi kutumia nyuklia katika utabibu- IAEA

10 Septemba 2018

Miradi ya pamoja kati ya shirika la kimataifa la atomiki, IAEA na nchi wanachama imesongesha matumizi ya sayansi ya nyuklia katika afya, kilimo na maeneo mengine lukuki.

Mkurugenzi mkuu wa IAEA, Yukia Amano amesema hayo wakati akifungua mkutano wa bodi ya magavana wa shirika hilo mjini Vienna, Austria.

Dkt. Amano ametolea mfano mataifa yanayoendelea ambayo amesema ataifa hivi sasa yanatumia sayansi ya nyuklia pamoja na teknolojia kutibu saratani.

“Madaktari wa saratani katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Mama Teresa huko Tirana, mji mkuu wa Albania sasa hivi wanatumia teknolojia ya juu kudhibiti saratani kuenea kwa mgonjwa na wamefanya hivyo kwa miaka 10 sasa nah ii ni kutokana na miradi sita inayotekelezwa kwa pamoja na IAEA.” Amesema Dkt. Amano.

Amewajulisha pia wajumbe wa bodi hiyo kuhusu hatua zinazochukuliwa na IAEA kuboresha maabara ya matumizi ya nyuklia huko Seibersdorf, karibu na Vienna, akisema kuwa kazi inaendelea vizuri wakati huu ambapo nishati hiyo itaendelea kuwa na dhima muhimu kwenye kusaidia kupunguza nishati zinazochafua mazingira.

Hata hivyo ameonya kuwa kuna mwelekeo wa kupungua kwa matumizi ya nishati salama ya nyuklia iwapo hakutakuwepo na juhudi za pamoja za kufanikisha matumizi sahihi na salama ya nishati hiyo.

“Itakuwa vigumu sana kupata nishati ya kutosha na kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Dkt. Amano akigusia suala hilo la athari za ukosefu wa ushirikiano.

Mkuu huyo wa IAEA pia amegusia ripoti ya usalama wa nyuklia yam waka 2018 inayotathmini kazi za shirika hilo kusaidia nchi kuwa na mifumo bora ya kuepusha nishati ya nyuklia kuangukia mikononi mwa magaidi.

Kuhusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini, Dkt. Amano ameeleza wasiwasi mkubwa juu ya nchi hiyo kukiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akitoa wito kwa nchi hiyo kuzingatia kwa kina wajibu wake na kushirikiana na IAEA katika kusaka suluhu ya mambo ambayo bado yana utata.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud