Wahalifu Libya msituchafulie jina:UNHCR

8 Septemba 2018

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia  wakimbizi la UNHCR, limetoa wito kwa serikali nchini Libya kuchukua hatua madhubuti dhidi ya wahalifu wanaowalenga  wakimbizi na wahamiaji wakati kukiwa na taarifa za kuwa wasafirishaji haramu  wa binadamu hujifanya kama wafanyakazi wa UNHCR.

 

Kwa mujibu wa shirika hilo duru za habari za kuaminika pamoja na ushahidi kutoka kwa wakimbizi zimearifu kuwa wahalifu hutumia vizibao pamoja na vifaa vingine vyenye nembo zinazofanana na za UNHCR katika vituo vya kushukia na katika vituo vya usafirishaji haramu.

UNHCR imeongeza kuwa wafanyakazi wake rasmi wapo katika sehemu za kushukia wakimbizi na wahamiaji nchini Libya  wakitoa msaada wa huduma za kiafya na kibinadamu kama vile chakula, maji,na nguo.

UNHCR inapinga hatua ya kuwaweka vizuizini  wakimbizi na wahamiaji lakini ina wafanyakazi wake ambao wanaangalia hali ya mambo inavyokwenda katika vituo hivyo nchini Libya huku ikitoa msaada kwa wale walioko taaban.

Hata hivyo shirika hilo linasisitiza kuwa halihusiki kamwe katika harakati zozote za kuwahamisha wakimbizi kutoka vituo vya kushukia.

Taarifa kuhusu wahalifu wanaojifanya kuwa watumishi wa UNHCR zinakuja wakati hali ya wakimbizi na wahamiaji walioko vizuizini inazidi kuwa mbaya nchini Libya. 

Kufuatia machafuko yaloyozuka mjini Tripoli Agosti 26 wakati vifaru na silaha zingine nzito zilipotumika katika maeneo ya raia, UNHCR imepokea taarifa za uhalifu dhidi ya wakimbizi na wahamiaji mjini Tripoli mkiwemo ubakaji,utekaji na kuteswa.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter