Leo ni siku ya kimataifa ya kufuta ujinga wa kutokujua kusoma na kuandika

8 Septemba 2018

Jumuiya ya kimataifa imeombwa kuchukua hatua za pamoja kuendeleza elimu na ujuzi katika vita dhidi ya kutojua kusoma na kuandika.

Wito huo umetolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO, wakati wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya kufuta ujinga wa kutokujua kuandika wala kusoma ambayo inasherehekewa kila mwaka tarehe 8 Septemba  duaniani kote.

Wito huu unakuja kukiwa na taarifa za watu milioni 750 duniani kote wasiojua kusoma wala kuandika na kati ya hao wote theluthi mbili ni wanawake ambao bado ni vijana.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni kuendeleza kujua kusoma na kuandika pamoja na ujuzi. Umoja wa Mataifa unasema siku hii ni fursa nzuri kwa wadau kumulika mabadiliko katika viwango vya kusoma na kuandika duniani na pia kutafakari changamoto zilizosalia kuhusu suala hili.

Umoja wa Mataifa unasema kusoma na kuandika ni kipengee muhimu cha  malengo ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu na pia ajenda ya Umoja wa Mataifa ya 2030.

 UNESCO  inasema kuna watu milioni 192 duniani hawana ajira na huhitaji elimu na ujuzi kuweza kujiendeleza kimaisha.

Nalo lengo namba 4 lina shabaha ya kuhakikisha kuwa  vijana  wengi wanapata elimu na watu wazima ambao hawana elimu kuwawezesha kuipata.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter