Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

La msingi ni kuanza kwa mjadala kuhusu suluhu ya Yemen: Griffins

Martin Griffiths,Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo wa Yemen.
UN Geneva/Violaine Martin
Martin Griffiths,Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo wa Yemen.

La msingi ni kuanza kwa mjadala kuhusu suluhu ya Yemen: Griffins

Amani na Usalama

Mjadala kuhusu kupata suluhu ya mzozo wa Yemen yameanza na ni hatua inayotia matumaini amesema mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo unaondelea nchini humo.

Martin Griffins akizungumza hii leo amekiri kuwa japo moja ya kundi muhimu la upinzani la Ansarulla-Houthi kutotokea katika mazungumzo yanayofanyika mjini Geneva Uswis hicho sio kikwazo kikubwa sana kwani “la msingi ni kuanza kwa majadiliano”. Kujenga mazingira ya kuaminiana kati ya pande zote katika mgogoro wa kisiasa uliozusha zahma kubwa ya kibinadamu na suluhu ya janga hilo ni lazima.

Ameongeza kuwa kuanza kwa mazungumzo hayo ni jambo la kutia moyo, kwani watu wa Yemen pamoja na jamii ya kimataifa wanataka afaulu katika mchakato huu wa kurejesha amani Yemen hivyo yuko tayari na atakutana na wawakilishi wa wa Houth Muscat, Oman na Sana’a mji mkuu wa Yemen miji ambayo wanadhibiti.

Ameeleza kuwa atahakikisha wanafanya mashauriano na Ansarullah na uzuri mmoja wa mashauriano  si lazima nyote muwe katika chumba cha mkutano pamoja au mji mmoja. Ameongea kuwa akiwa Oman kukutana na wawakilishi wa Houthi atawafahamisha waliyojadilia Uswisi na kusikiliza  wanasema nini, akisisitiza kuwa ujumbe wa Houthi uko tayari kushiriki katika mchakato wa kisiasa ambao umeandaliwa na Umoja wa Mataifa.

Jambo la msingi amesema endapo Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na yeye mwenyewe wasingedhani kwamba kuna uwezekano wa kupatikana kwa suluhu Yemen wasingepoteza muda wao kuchagiza mchakato huu, lakini ana imani kuwa amani ya kudumu Yemen inawezekana kwa ushiriki wa wadau wote.