Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto zaidi ya milioni 1 maisha yao yako hatarini Idlib Syria:UNICEF

Mtoto akiwa ameketi kwenye dawati ndani ya moja ya darasa la shule iliyoshambulia huko Idleb nchini Syria mwaka 2016
UNICEF
Mtoto akiwa ameketi kwenye dawati ndani ya moja ya darasa la shule iliyoshambulia huko Idleb nchini Syria mwaka 2016

Watoto zaidi ya milioni 1 maisha yao yako hatarini Idlib Syria:UNICEF

Amani na Usalama

Kuongezeka kwa mapigano zaidi huko Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria, kutaweka hatarini maisha ya watoto zaidi ya milioni 1, Shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema hii leo.

"Maelfu ya watoto mjini Idlib wamelazimika kukimbia makwao mara nyingi na sasa wanaishi katika makazi yaliyofurika, pamoja uhaba wa chakula, maji na dawa," amesema Henrietta Fore, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEFakiongeza kuwa "Wimbi jipya la unyanyasaji linaweza kuwakwamisha katika eneo la mapigano na hivyo kuleta zahma kubwa zaidi."

Maisha ya watoto mjini Idlib yako hatarini kila siku hata kama wanajaribu kuzifikia huduma za kiafya na elimu ambazo tayari ni hafifu. Ni takribani nusu ya vituo vya afya vya umma vinavyofanya kazi hivi sasa, na madaktari wanasema hawana dawa muhimu na vifaa.

Kuongezeka kwa mapigano pia kunaweza kusababisha shule kufungwa na watoto kubaki nyumbani. Hata ambapo mwaka mpya wa shule umeanza Septemba mosi, shule nyingi bado hazina vifaa muhimu, karibia madarasa 7,000 yanahitaji kurekebishwa na zaidi ya nafasi 2,300 za walimu ziko wazi.

Wakati mapigano yanavyoongezeka, UNICEF inaguswa na hali kuwa mashambulizi mazito ya anga, shughuli za kijeshi za ardhini, na matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye wakazi wengi yatakuwa hatarishi kwa watoto. Kama tulivyoona nchini Syria, watoto ndiyo huathirika zaidi kwa kupoteza elimu, afya, akili na kimwili, na maisha yao.

UNICEF inarudia tena wito kwa pande zote zinazohusika na mgogoro kuzingatia wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya haki za kibinadamu.

"Ombi letu ni rahisi: Linda watoto. Tupeni fursa salama, endelevu na isio na masharti kuwafikia. Ruhusu na wezesha wale ambao wanataka kuondoka kufanya hivyo kwa usalama na kwa hiari, "amesema Fore.

Wakati upatikanaji wa huduma za kibinadamu ni mdogo, UNICEF inafanya kazi na washirika wake wa hapo Idlib, magharibi ya Aleppo na kaskazini mwa Hama kutoa msaada wa kuokoa maisha na kukabiliana na kuhamisha raia. Hii ni pamoja na kutoa maji, usafi wa mazingira, usafi, afya, lishe, huduma za ulinzi, elimu na vifaa.

Bi. Fore ameongeza kuwa  "Wakati Baraza la Usalama hii leo linashiriki mashauriano ya Syria, ninawakumbusha wanachama wake kwamba siku zijazo za mamilioni ya watoto wa Syria ziko mikononi mwao,". Kama yalivyo  mashirika mengine ya kibinadamu, tunafanya kila tuwezavyo, lakini hii haitoshi. Ni wakati sasa mataifa kuzingatia wajibu wao kuhusu  watoto