Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukandamizaji wa maandamano ya amani DRC unatoa hofu:UN

Vyomb vya dola wakati wa maandamano ya mjini Kinshasa
MONUSCO
Vyomb vya dola wakati wa maandamano ya mjini Kinshasa

Ukandamizaji wa maandamano ya amani DRC unatoa hofu:UN

Haki za binadamu

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema itatiwa hofu kubwa na vitendo vya ukandamizaji na ghasia dhidi ya maandamano ya amani yanayofanywa na mashirika ya kiraia na upande wa upinzani wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Kwa mujibu wa ofisi hiyo ya haki za binadamu haya yanafanyika, licha ya ahadi ya uongozi wa DRC iliyowekwa tangu mwaka 2017 ya kufuta marufuku ya awali ya watu kutoruhusiwa kuandamana.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswis Ravina Shamdasani msemaji wa ofisi hiyo ameongeza kuwa wakati hali ya kuimarika imeanza kuonekana katika udhibiti wa mikusanyiko ya watu na ufuataji wa sheria na na usalama, jeshi la polisi la DRC limeendelea kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wanaharakati wa kisiasa na waandamanaji hali iliyosababisha mauaji ya mwanaharakati mmoja wa kisiasa Kusini Mashariki mwa nchi hiyo na kukamatwa kwa makumi wengine.

Amesisitiza kuwa kabla ya kuelekea katika uchaguzi mkuu muhimu chini DRC unaotarajiwa hapo Desemba 23 mwaka huu, “tunautaka uongozi wa Congo kuzingatia haki za uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani. Madai yoyote ya matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na polisi na vikosi vingine vya usalama ni lazima yachunguzwe kwa mtazamo wa kuwawajibisha wahusika.”

Na pia amesema haki inasalia kuwa muhimu kwa wahanga wa matukio ya nyuma ya mauaji na kujeruhiwa yaliyosababishwa na matumizi ya nguvu kupita kiasi ambayo yalitekelezwa na vikosi vya ulinzi na usalama katika maandamano wa 2016.

Hivyo amerejea kusema Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia mipango yote itakayochangia kuwafikisha kwenye mkono wa sheria wahusiaka wa ukiukwaji wa haki za binadamu nchini DRC.