Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani Somalia inahitaji wadau wote kuaminiana: Keating

Raia wa Somalia wakiwa wamesimama nje ya kioski eneo la soko katika bandari ya Kismayo, Kusini mwa Somalia.
UN Photo/Stuart Price
Raia wa Somalia wakiwa wamesimama nje ya kioski eneo la soko katika bandari ya Kismayo, Kusini mwa Somalia.

Amani Somalia inahitaji wadau wote kuaminiana: Keating

Amani na Usalama

Viongozi wa majimbo mbalimbali nchini Somalia wamehimizwa kuimarisha ushirikiano baina ya serikali zao na serikali kuu kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kuuweka mazingira ambayo yatakuwa ya manufaa kwa wasomali wote.

Wito huo umetolewa na Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Michael Keating, mjini Kismayo wakati wa mkutano wa baraza la ushirikiano wa majimbo CIC ambao umewaleta pamoja  viongozi wa majimbo ya Puntland, HirShabelle, Galmudgud, na yale ya Kusini Magharibi.

Lengo la mkutano huo ni kujadili mbinu za kuendeleza ushirika miongoni mwa majimbo tofauti nchini humo. Bwana Keatinging akihimiza ushirika huo kwa ajili ya maendeleo  amesema

Kwa maoni yangu matatizo ya Somalia, ama yanauhusiiano na umaskani au mabadiliko ya hali ya hewa, uwezo wake wa  kuvutia wawekezaji na kutatua migogoro unategemea sana viongozi wa kisiasa nchini humo  kuweza kuaminiana na kukubali ajenda moja. Kwa hivyo hii ni sehemu moja muhimu ya hali halisi.”

Ameongeza kuwa bila ya hao Somalia iko mashakani na yakiwepo ni ushindi kwa pande zote   ikiwemo mamilioni ya watu ambao wanastahili maisha bora, kwani mafanikio yanategemea uwepo wa imani na hatua za pamoja kutoka kwa serikali kuu na wajumbe wa serikali hiyo.

Mjumbe maalum amekariri kuwa  mkutano wa Kismayo unatoa nafasi ya mambo kusogea mbele katika njia sahihi.

Masuala mengine yaliyojadiliwa na viongozi hao ni  mabadiliko ya katiba ya nchi, mfumo wa sheria, upitishwaji wa sheria za uchaguzi na pia makubaliano ya kugawana mapato.

Mjini Kismayo pia kuna kituo cha wakimbizi wanaorejea nyumbani ambacho kinafadhiliwa na  shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCRkwa ubia na asasi ya kiraia ya , Mercy Corps, . Na kinapokea wakimbizi wa Somalia wanaorejea kutokea Kenya, hususan kutoka kambi ya Dadaab iliyo na wakimbizi na wasaka hifadhi  waliosajiliwa takriban 200,000.