Tunakaribisha hatua ya kukamilisha uchunguzi wa mauaji ya MacDonald Malawi:UN

5 Septemba 2018

Uchunguzi wa kesi ya mauaji ya mtu mwenye ulemavu wa ngozi au Albino umekamilika nchini Malawi na watu 12 wanakabiliwa na mashitaka ya kuhusika na kesi hiyo ikiwemo mauaji.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Malawi imekaribisha hatua ya kukamilika kwa uchunguzi wa kesi hiyo ya mauaji dhidi ya  MacDonald Masumbuka.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo ofisi hiyo inasema washukiwa 12  akiwemo afisa wa polisi, daktari na kuhani au padre, wananza kujitetea katika mashitaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na mauaji na kusababisha madhara kwa watu wenye ulemavu.  Umoja wa Mataifa umesema “Tunatoa wito kwa Serikali ya Malawi kuwashtaki na kuwahukumu haraka watuhumiwa wa madai katika kesi hii ya kihistoria.”

Umoja huo umesema pia , una wasiwasi na kuendelea kwa mashambulizi dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi huku ikielezwa kuwa mwaka huu pekee watu 10 wenye ulemavu wa ngozi  wametoweka na hawajulikani waliko akiwemo kijana wa miaka 12 Joseph Kashingwe ambaye alipotea Julai 2018 katika eneo la Phalombe baada ya kuhudhuria sherehe za Uhuru.

Na Agosti 16  mwaka wa 2018, mtoto mvulana wa umri wa miaka mitano mwenye ulemavu wa ngozi aliponea chupuchupu kutekwa katika sehemu za Chikwawa.

 Umoja wa Mataifa  unatoa wito wa kuwaongezea ulinzi kwa waathirika pamoja na familia zao na pia kuongeza uhamasishaji kwa jamii ukiambatana na mpango kazi wa kitaifa kuhusu watu wenye ulemavu wa ngozi wa mwaka 2018-2022.

Umetoa wito kwa serikali ya Malawi kuharakisha uchunguzi na kuwafungulia mashtaka wahusika wa ukatili na mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa kuzingatia ahadi iliyotolewa kwenye mkutano wa ngazi ya juu kuhusu watu wenye ulemavu wa ngozi uliofanyika mjini Lilongwe Juni  2018.  Hadi sasa ni kesi 45 tu za makosa ya jinai dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi ambazo zimefika mahakamani kati ya kesi zote 145. Ni kesi moja tu ambayo imekamislishwa katika mahakama ya juu.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud