Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wazima zaidi ya bilioni 1 hawashughulishi viungo vya mwili:WHO

Wasichana wanafanya mazoezi wakicheza huku wakikimbia huku na kule
UNICEF/Vishwanathan
Wasichana wanafanya mazoezi wakicheza huku wakikimbia huku na kule

Watu wazima zaidi ya bilioni 1 hawashughulishi viungo vya mwili:WHO

Afya

Zaidi ya watu wazima bilioni 1.4 duniani walibainika kutofanya mazoezi ya kutosha ya viungo vya mwili mwaka 2016 na kuwaweka katika hatari kubwa ya maradhi, imeonya ripoti ya shirika la afya duniani, WHO iliyochapishwa leo na jarida la afya The Lancent. 

Kwa mujibu wa utafiti huo wa kwanza kabisa duniani kukadiria mwenendo wa dunia katika masuala ya mazoezi ya viungo,  hatari inayowakabili watu kwa kutofanya mazoezi ya viungo ni pamoja na maradhi ya moyo, kisukari aina ya 2, magonjwa ya akili na baadhi ya aina za saratani. Dr Regina Guthold, mwana sayansi wa WHO na mwandishi mkuu wa utafiti huo amesema walichokuwa wanatafuta ni kufahamu kiwango cha kimataifa na kikanda kutofanya mazoezi ya viongo 

“Tumebaini kwamba zaidi ya robo ya watu wote duniani hawajishughulishi na mazoezi ya viungo.Na hali hii sio sawa kati ya wanaume na wanawake.Tuna asilimia 23 ya wanaume ambao hawafanyi mazoezi ukilinganisha na asilimia 32 ya wanawake.”

 Ameongeza kuwa na hili ni tatizo kwani mazoezi yanasaidia kuboresha afya, wakati kinyume chake ni kuongeza hatari ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama ya moyo, kiharusi, satarani za matiti na utumbo, shinikizo la damu na presha. Pia amesema kuna tofauti baina ya walionacho na hohehahe 

“Nchi zote za kipato cha chini kwa pamoja zilikuwa na kiwango cha asilimia 16 cha kutokuwepo na mazoezi ya kutosha , nchi za kipato cha wastani kiwango cha asilimia 28 na zile tajiri asilimia 37, hivyo tunaona wazi mwenendo hapa, kuwa nchi tajiri zina kiwango kikubwa cha watu kutojishughulisha na mazoezi ya viungo.”

 Naye Dr Fiona Bull meneja mradi , ufuatiliaji, na kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukiza kutoka WHO ameongeza kuwa kujishughulisha na mazoezi ya viungo vya mwili kuna faida kubwa

“Yanaboresha afya ya akili na maisha kwa ujumla, yanaweza kusaidia watu kujifunza, kufanya kazi vizuri na kuzuia kuanguka. Hivyo katika maisha yote kuanzia utotoni, mazoezi yanafaida za kiakili, kimwili na kiafya.”

Mataifa mbalimbali yameshirikishwa katika tathimini hiyo yakiwemo 41 ya Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara yanayojumuisha Tanzania, Kenya, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.