Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto Zaidi ya milioni 3 hatarini kukosa elimu, Ziwa Chad

Mgogoro wa bonde la Ziwa Chad
OCHA
Mgogoro wa bonde la Ziwa Chad

Watoto Zaidi ya milioni 3 hatarini kukosa elimu, Ziwa Chad

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, limetoa ombi la dola milioni 41.7 ili kushughulikia mahitaji ya elimu kwa watoto walioathiriwa na mzozo katika eneo la Ziwa Chad.

Ombi hilo limetolewa kwenye mkutano wa siku mbili mjini Berlin, Ujerumani unaohudhuriwa na mashirika ya kimataifa, serikali na asasi za kiraia  ukiwa na lengo la kusaka michango zaidi ya kibinadamu kwa ajili ya  wathirika wa mzozo katika bonde la Ziwa Chad.

Kwenye mkutano huo unaokunja jamvi leo, UNICEF imeonya kuwa mzozo unaoendelea, ukilazimisha watu kukimbia makwao na kuhatarisha shule kushambuliwa unatishia fursa ya elimu kwa watoto zaidi ya milioni 3.5, hasa wakati huu ambapo takribani shule 1,000 zimefungwa kaskazini Mahsariki mwa Nigeria, Chad, Cameroon na Niger.

Manuel Fontaine, Mkurugenzi wa mipango ya dharura ya UNICEF amesema  wakati wa mizozo, elimu yaweza kusaidia maisha kuendelea na kuwa mwokozi wa maisha kando na kutoa fursa za elimu ya maisha kwa watoto.

Ameongeza kwamba elimu huwapatia ujuzi unaofaa kuwasaidia kujenga mustakbali wao na familia zao kinachochangia kwa ujenzi wa amani na uwepo wa jamii endelevu.

Fontaini amesema licha ya umihimu wa elimu, ufadhili wa kibinadamu katika sekta hiyo mara nyingi huwa finyu wakati wa dharura.

Naye Marie-Pierre Poirier, Mkurugenzi wa kanda ya Afrika Magharibi na Kati wa UNICEF, amezitolea wito nchi kutia saini mkataba wa Shule Salama na kuweka mikakati ya kuhakikisha usalama wa watoto shuleni hata wakiwa mzozoni.

Ingawa hali ya usalama imeimarika katika Bonde la Ziwa Chad, watu zaidi ya milioni 10 wakiwemo watoto milioni 6 bado wanahitaji misaada ya kibinadamu huku wengine milioni 2.4 waliolazimika kukimbia makwao.

Wakati wa kufunga mkutano huo mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kuratibu masuala ya kibinadamu Mark Lowcock amesema zaidi ya dola bilioni moja zinahitakika ili kulinusuru eneo hilo la Chad na changamoto mabalimbali ikiwemo za misaada ya kibinadamu na huduma muhimu kama kuboresha elimu.