Miaka saba jela dhidi ya waandishi wa Reuters Myanmar haistahili: UN

3 Septemba 2018

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa  wamelaani vikali hatua ya mahakama  nchini Myanmar kuwahukumu kwenda jela waandishi wa habari wawili wa shirika la habari la Reuters.

Waandishi habari hao, Wa Lone na Kyaw Soe Oo wamekatiwa kifungo cha miaka saba kila mmoja na mahakama ya Yangon kwa kosa la kukiuka sheria zinazohusu siri za nchi kwa kuripoti kuhusu jimbo la Rakhine.

Wataalam hao, David Kaye anayehusika na kuchagiza haki za uhuru wa kujieleza na uhuru wa maoni na mtaalam maalum kuhusu haki za binadamu nchini Mynamar, Yanghee Lee, wamesema hukumu dhidi ya waandishi hhao wawili wa habari ni ishara ya wakati wa giza kwa Myanmar.

Wameongeza kuwa hii ni Ishara nyingine bayana ya Myanmar kuendelea kujitenga na sheria za kimataifa za haki za binadamu. “tunasikitika kwamba mahakama imeshindwa kutambua umuhimu wa uhuru wa waandishi wa habari uhuru wa kujieleza na haki ya umma kupata taarifa.”

Wametoa wito kwa rais  kuwasamehe waandishi hao, na endapo kutakuwa na kukata rufaa mahakama izingatie  wajibu wa  Myanmar kuhusu haki za binadamu na kuamuru waachiiwe huru.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud