Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wamekuwa wahanga wakubwa wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani:UNICEF

Watoto walicheza katika eneo lililokumbwa na mafuriko Maiduguri jimboni Boeno Kaskazini mashariki mwa Nigeria.
UNICEF/Fati Abubakar
Watoto walicheza katika eneo lililokumbwa na mafuriko Maiduguri jimboni Boeno Kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Watoto wamekuwa wahanga wakubwa wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani:UNICEF

Tabianchi na mazingira

Matukio mengi ya hali mbaya ya hewa duniani yakiwemo mafuriko kusini mwa India, moto nyikani huko magharibi mwa Marekani na joto la kupindukia katika eneo la kaskazini mwa dunia, yanawaweka watoto katika hatari na kutishia hatima yao, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,  UNICEF imeonya hii leo.

“Katika kila janga, watoto ni miongoni mwa walio hatarini zaidi, na matukio ya hali mbaya ya hewa tunayoyashuhudia duniani kote ni sehemu ya sababu za hatari” Amesema Ted Chaiban, Mkurugenzi wa Programu katika shirika hilo.

Mwezi Juni na Julai mwaka huu kulishuhudiwa kiwango kikubwa cha joto katika ukanda wa kaskazini mwa dunia, shirika la hali ya hewa la dunia (WMO) liliripoti miezi sita ya kwanza ya mwaka 2018 ilikuwa ya joto zaidi kuwahi kutokea duniani.

Kuanzia Amerika Kaskazini hadi Asia ya Mashariki na kutoka Kaskazini mwa ncha ya dunia hadi Ulaya, eneo kubwa la dunia limeghubikwa na fukuto la joto, ukame, mioto ya nyika, mafuriko na maporomoko ya ardhi, vyote vikisababisha majeraha, vifo, na uharibifu wa mazingira ikiwemo kupoteza mazao.

Ingawa tukio mojamoja la hali ya hewa haliwezi kuhusishwa moja kwa moja na mabadiliko ya tabia nchi, kuongezeka kwa matukio ya hali mbaya ya hewa na viwango vyake vinaweza kuwa viashiria vya namna gani shughuli za kibinadamu zinaathiri hali ya hewa ya dunia.

UNICEF inasema matukio hayo yanaweza kuchangia kuongezeka kwa vyanzo vya vifo vya watoto kama utapiamlo, malaria na kuhara.

 “Kadri dunia inavyoshuhudia mabadiliko ya tabia nchi, ni maisha ya watoto na hatima yao ambavyo vitavurugwa zaidi” ameongeza Chaiban. “Kwa hivyo, ni muhimu Serikali na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti kulinda mstakabali wa watoto na haki zao. Matokeo mabaya zaidi ya mabadiliko ya tabia nchi hayaepukiki lakini wakati wa kuchukua hatua ni sasa”

Tafiti nyingi zimeonesha kuwa mabadiliko ya tabia nchi yaliyosababishwa na binadamu yamechangia ongezeko la matukio na wingi wa joto duniani. Watoto wako hatarini zaidi hasa walio chini ya umri wa miezi 12. Vichanga na watoto wadogo wako hatarini kupoteza maisha au kuzirahi kunakotokana na joto kwa kuwa hawana uwezo wa kuhimili joto lao la mwili na mazingira yanayowazunguka. Pia hali ya joto kubwa zaidi inaongeza umuhimu wa maji safi na salama ilihali katika mazingira mengi maji yanapotea kutokana na joto na ukame.

Mafuriko yanatishia maisha na mendeleo ya watoto kwa athari za moja kwa moja ikiwemo majeraha na vifo kutokana na kuzama. Mafuriko piayanachafua maji salama na kuathiri hali ya usafi, kuongeza hatari ya magonjwa ya kuhara na milipiko ya magonjwa mengine ya kuambukiza lakini pia yanaathiri elimu.

Ukame una matokeo kadhaa kwa familia na jamii maskini. Kuharibika kwa mazao, kufa kwa mifugo na kushuka kwa kipato, vyote hivihusababisha baa la njaa kwa maskini pamoja na kuongeza bei ya vyakula duniani.

Agenda za UNICEF kuhusu hatua dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi ni pamoja na: Kuimarisha miundombinu ya afya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuongeza udhibiti dhidi ya wadudu wasambazao magonjwa, kusambaza chanjo na kusisitiza ujenzi wa majengo yanayowezakuhimili majanga.

Pia kuongeza uwekezaji zaidi katika mazao yanayoweza kuhimili mabadiliko ya tabia nchi, Kuwapa vijana na watoto elimu kuhusu mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuweka njia za kuwalinda watoto ambao wamepoteza makazi, kuhamishwa au kuwa wakimbizi kutokana na mabaadiliko ya tabia nchi na matokeo mengine yanayochangiwa na hali hiyo.

TAGS: UNICEF, WMO, watoto, mabadiliko ya tabia nchi, mafuriko, joto