Waathirika wa mashambulio ya Tripoli wapata msaada: IOM

31 Agosti 2018

Katika kuitikia mahitaji ya mamia ya wahamiaji na Walibya walioathiriwa na mapigano yaliochacha mjini Tripoli mapema wiki hii, ShirIka la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM  katika ushirikiano na wahudumu wengine wa kibinadamu wamefanikiwa kurejesha makwao watu zaidi ya mia moja kando na kutoa msaada wa dharura.

Othman Belbeisi, Mkuu wa ujumbe wa IOM nchini Libya ameelezea idhaa hii kuwa, kati ya changamoto za kiusalama, walifanikiwa, kusafirisha watu 164 wakiwemo watoto wachanga wawili na watu wengine wanane waliokuwa katika uhitaji wa tiba, hadi kwenye uwanja wa ndege wa Mitiga ili waweze kuendelea na safari ya nyumbani kwao nchini Mali.

Mafanikio haya ya tarehe 28 Agosti ni matunda ya juhudi za IOM ikishirikiana na mamlaka ya serikali za Mali na Libya.

Kwa sasa mashirika ya kibinadamu yanapanga mikakati ya kurejesha nyumbani kwa hiari  Wasomali zaidi ya 90 walioathiriwa na mapigano haya.

Mapigano makali yalizuka katika mji mkuu wa Libya, Tripoli hapo Jumatatu kati ya vikundi hasimu vilivyojihami na kulazimisha wananchi na wahamiaji wengi kukimbia makwao katika maeneo yalioathirika.

Blanketi 500 chakula na vinywaji ni sehemu ya msaada uliotolewa kwenye kizuizi cha Abu Slim na wahamiaji zaidi ya 400 wakiwemo 322 walioondolewa katika maeneo yasio salama.

Wadau wakibinadamu wanoshirikiana na IOM ni pamoja na shirika la Umoja wa  Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na shirika la madaktari wasio na mipaka, MSF.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter