Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia yaweza kuwa mkombozi wa maendeleo duniani:FOSS4G 2018

Drone ya UN.
Photo: MONUSCO/Abel Kavanagh
Drone ya UN.

Teknolojia yaweza kuwa mkombozi wa maendeleo duniani:FOSS4G 2018

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa kimataifa wa kutumia ubunifu wa ramani mtandaoni kufuatia picha zilizopigwa na ndege zisizokuwa na rubani au drones, unaendelea hivi sasa jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, ukiwaleta pamoja wadau zaidi ya1000 kutoka nchi mbalimbali duniani.  

Mkutano huo ujulikanao kama FOSS4G 2018, unajumuisha wataalamu wa ramani mtandaoni, wawakilishi wa serikali mbalimbali, sekta binafsi, vyuo, vijana, na taasisi zisizokuwa za kiserikali.

Mkutano huo ulioandaliwa na FOSS4G, Benki ya Dunia, Umoja wa Mataifa na wadau wengine, unatoa fursa kwa washiriki  kubadilishana mawazo kuhusu umuhimu na faida ya kutumia teknolojia kuleta maendeleo na kuboresha kanzi data. Miongoni mwa washiriki ni Khadija Abdullah Ali  alimaarufu kama Malkia wa Drone kutoka Zanzibar, yeye ni mtaalam wa kutengeneza ramani kwa kutumia teknolojia ya ndege zisizo na rubani au Drones anaeleza kwa nini ni muhimu kutumia teknolojia hizo kwa ajili ya kuleta maendeleo katika jamii.

SAUTI YA KHADIJA ABDULLAH ALI 

Kwa mujibu wa waandaji wa mkutano huo kanzi data ni tatizo kubwa katika  nchi nyingi barani Afrika na duniani kote, hivyo uwezo wa kupata taarifa za msingi utasaidia kupima maendeleo kwa siku zijazo.

Hii ni mara ya pili mkutano huu wa kimataifa unafanyika barani Afrika.Mara ya kwanza ulifanyika nchini Afrika Kusini mwaka 2016, na mwaka huu Tanzania. Mkutano huo wa siku sita utakunja jamvi tarehe 3 Septemba.