Kila nchi duniani ni lazima ichukue hatua haraka kuwatafuta watu ambao walitoweshwa kwa lazima na kuhakikisha uhalifu huo unachunguzwa kikamilifu na hatua kuchukuliwa.
Wito huo umetolewa mjini Geneva Uswisi na wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya waathirika wa kutoweshwa kwa lazima ambayo kila mwaka hufanyika Agosti 30.
Katika taarifa yao, watalaam hao wamesema ndugu wana haki kama walivyo waathiriwa wenyewe ya kujua ukweli wa mazingira yaliyosababisha kutoweka kwa wapendwa wao, kujua mchakato wauchunguzi, matokeo ya uchunguzi na hatimaye mustakhbali wa watu waliotoweka.
Kwa mujibu wa wataalamu hao “Hatua za kufikia ukweli na haki kwa watu waliotoweshwa kwa lazima ni sharti ziende sambamba, kwani hakuna ukweli bila haki na hakuna haki bila ukweli”
Mwenyekiti wa kamati ya watu kutoweshwa ,Suela Janina, amesisitiza kuwa kutafuta waliotoweka ni haki za waathirika na pia wajibu wa nchi na kunapaswa kufanywa kwa nia njema na utaratibu muafaka.
Ameongeza kuwa kwa mataifa yote yaliyoridhia mkataba wa kupinga watu kutoweshwa kwa lazima inafaa zianze haraka kuwasaka watu hao na pia zinapaswa kuweka será za kusaidia utafutaji wa watu hao kwa kuwashirikisha kwa karibu ndugu na jamaa zao.
Naye mwenyekiti wa kundi la wawakilishi maalumu kuhusu suala hili,Bernard Duhaime, amesema endapo viwango vya kimataifa vitanoa mwongozo ili kuwa na mfumo wa kisheria wa jinsi gani ya kuchunguza visa vya watu kutoweshwa nchi zinapaswa kutekeleza wajibu wake kwa vitendo na ni lazima udadisiwe kwa kina.