Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asante Benki ya Dunia kwa kunitoa katika umasikini:

Mama akiwa na watoto sita aomba msada nchini Yemen.
UNICEF
Mama akiwa na watoto sita aomba msada nchini Yemen.

Asante Benki ya Dunia kwa kunitoa katika umasikini:

Wanawake

Kutana na Fatima Haja, mkulima kutoka Yemen ambaye baada ya mumewe na mwanaye mkubwa wa kiume kufariki dunia alilazimika kubeba jukumu la kulea familia peke yake na kibarua hicho hakikuwa rahisi. Sharifa Kato mwanafunzi wa mafunzo ya vitendo hapa kwenye Umoja wa Mataifa anasimulia safari ya mama huyo.

Bi Haja mbali ya kuwajibika kulea na kulisha watoto wengine sita waliosalia na yeyé mwenyewe, ilimbidi pia kushika usukani wa kuendesha shamba la famila,  mtihani uliokuwa mkubwa hasa kwa nchi ya Yemen ambayo imegubikwa na vita.

Alihangaika sana na vita vilipozidi kuchachamaa hakuwa na jinsi bali kulazimika kuacha kilimo hatua iliyomuacha mtupu, bila kipato chochote na hakuweza tena kununua hata mahitaji muhimu wala kulisha familia.

Pamoja na mtihani huo Fatima hakukata tamaa alitaka kufufua tena shughuli za kilimo, na baada ya dhiki kweli ni faraja, kwani nuru ilimuangazia kupitia mradi wa Benki ya Dunia wa kusaidia kwenye migogoro na na ule wa huduma ya miradi midogomidogo ujulikanao kama (SMEPS).

 

Mkulima akitayarisha shamba lake kama sehemu ya mradi wa FAO nchini Yemen
FAO/Soliman Ahmed
Mkulima akitayarisha shamba lake kama sehemu ya mradi wa FAO nchini Yemen

 

Fatima akaweza kupata ufadhili uliojumuisha mitambo ya umwagiliaji, mbegu na mbolea, na ukamsaidia kuanza tena shughuli za kilimo na kuweza kumpatia kipato. Ufadhili huo uligharimu dola 1, 500.

Kwa kutumia teknolojia hiyo mpya Fatima ameweza kuzalisha mazao mengi zaidi na kuongeza pato la familia yake. Akiwa na furaha kubwa anasema“msaada huu umenipa matumaini na nguvu ya kuendelea kulima na kulea familia yangu.”

Hivi sasa si haba , Fatima anapata kiasi cha Rial za Yemen 80,000 kila msimu fedha zinazotosheleza kumlisha yeye, familia yake na kuendeleza kilimo.