Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafunzo ya lugha ya Kingereza yawa mkombozi kwa wanawake Abyei:IOM

Wanawake waliohitimu mafunzo ya lugha ya kingereza yaliyotolewa na IOM, Abyei
IOM/A. Deng 2018
Wanawake waliohitimu mafunzo ya lugha ya kingereza yaliyotolewa na IOM, Abyei

Mafunzo ya lugha ya Kingereza yawa mkombozi kwa wanawake Abyei:IOM

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mafunzo  ya lugha ya Kingereza yanayotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji,  IOM kwenye jimbo la Abyei yamekuwa mkombozi mkubwa kwa wanawake hasa katika kujikimu kiuchumi. 

IOM imetoa mafunzo haya kwa kuitikia ombi la wanawake wa Abyei kuelimishwa lugha ya Kingereza ili waweze kushiriki katika mchakato wa maendeleo hasa katika biashara wakifahamu kuhesabu fedha, kuandika na kusoma na hatimaye waweze kuajiriwa na mashirika ya kimataifa ambako ujuzi wa Kingereza ni sifa muhimu.

IOM ilianza kuelimisha wanawake hao mnamo Februari mwaka huu wa 2018 katika ushirikiano na kampuni ya Rayons Consult ya Sudani Kusini kwa msaada kutoka Mfuko wa ufadhili wa Kimataifa wa Marekani, kama elimu ya watu wazima, FAL

Wanafunzi zaidi ya 314 wakiwemo wanawake  292 tayari wamemaliza kozi zao na kuhitimu mnamo mwezi huu wa Agosti. Ali Bunyenyezi wa Rayons Consult ambaye ni Mkufunzi wao amesema, wanawake hao walikuwa na dhamira ya kuelimishwa na pia walionekana wakijihisi kuwa wamewezeshwa kabisa na ujuzi huo mpya.

Elimu hii ya watu wazima ni sehemu ya mradi kabambe unaotekelezwa na IOM kwa madhumuni ya kuwezesha wanawake katika Jimbo la Abyei.

Mifumo ya elimu katika eno la Abyei ambalo limekuwa likizozaniwa baina ya Sudan na Sudan Kusini ilivunjika kati ya mwaka 2008 na 2011 wakati makombora yakivurumishwa na kulazimisha watu wengi kukimbia makwao, wathirika zaidi wakiwa ni wanawake.

Idadi kubwa ya wanawake katika Jimbo la Abyei nchini Sudan Kusini hawajapata fursa ya kuhudhuria shule na hata waliobahatika kuhudhuria waliaacha kusoma kabla ya kumaliza shule ya msingi wakijikuta wakiwa wahanga wa mimba na ndoa za utotoni.