Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlinda amani auawa CAR, UN yanena

Kofia ya chuma  ya buluu na vizibao mahsusi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa
UN /Marie Frechon
Kofia ya chuma ya buluu na vizibao mahsusi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa

Mlinda amani auawa CAR, UN yanena

Amani na Usalama

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa waendelea kulengwa kwenye mashambulizi katika nchi ambako wamejitolea kwenye kusaidia kuwepo kwa amani ya kudumu.

Umoja wa Mataifa umelaani vikali shambulio dhidi ya msafara wa walinda amani huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR lililosababisha kifo cha mlinda amani kutoka Burundi.

Walinda amani hao walioko kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini CAR, MINUSCA walishambuliwa na wanamgambo wa Anti-Balaka kwenye kijiji cha Pavika kilichoko jimbo la Basse-Kotto kusini-mashariki mwa nchi hiyo wakati walipoenda kuweka doria.

Kwa mujibu wa MINUSCA mlinda amani huyo aliuawa wakati wanajibu mashambulizi kutoka kwa Anti-Balaka.

Kufuatia taarifa hizo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia msemaji wake ametuma rambirambi kwa familia ya mlinda amani huyo pamoja na serikali ya Burundi.

Mlinda amani wa UN akiwa kwenye doria katika viunga vya mji mkuu wa CAR, Bangui
UN/Eskinder Debebe
Mlinda amani wa UN akiwa kwenye doria katika viunga vya mji mkuu wa CAR, Bangui

Amerejelea kwamba mashambulizi ya makusudi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuwa uhalifu wa kivita na kwamba vikwazo vinaweza kuwekewa wahusika wa kitendo hicho.

Bwana Guterres ametoa wito kwa mamlaka za CAR zichunguze haraka kisa hicho na wahusika wafikishwe mbele ya sheria.
Halikadhalika amesisitiza msaada wake kwa MINUSCA ili iendelee kulinda raia na kuweka utulivu nchini CAR.

BARAZA LA USALAMA

Wakati huo huo, wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nao wametoa taarifa yao ambapo pamoja na kutuma salamu za rambirambi kwa wafiwa na serikali ya Burundi, wamelaani shambulio hilo na kutaka wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Wamesisitiza uungwaji wao thabiti wa mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini CAR Parfait Onanga-Anyanga, sambamba na MINUSCA katika kusaidia juhudi za mamlaka za  nchi hiyo na raia wake katika kusaka amani ya kudumu kwa mujibu wa azimio namba 2387 la baraza hilo.