Ubia wa UN na NGOs ni muhimu ili kufanikisha SDGs - Byanyima

22 Agosti 2018

Mkutano wa 67 kati ya asasi za kiraia, NGOs, na Idara ya mawasiliano ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa unaanza leo kwenye  makao makuu ya Umoja huo jijini New York Marekani ukilenga kusaka mbinu bora za pande mbili hizo kushirikiana ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Mwenyekiti wa mkutano huo ni Winnie Byanyima kutoka Uganda ambaye akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa amesema mkutano  huo ni muhimu kwa kuwa asasi za kiraia zina mchango adhimu.

 “Mchango muhimu kabisa. Katiba ya Umoja wa Mataifa  inaanza na sentensi , “ Sisi watu…”na tunataka kusogeza karibu hiyo kauli ya, “ sisi watu…”  sauti za wananchi. Mchango wetu ni kuhamasisha wananchi kupaza sauti kuhusu masuala yanayowahusu mbele ya watawala walio na uwezo, iwe serikali au mashirika na hii ndio nafasi muafaka.”

 

Wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Weruweru nchini Tanzaniwa wakiwa wamebeba mabango ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kutoka namba 1 hadi 5. (Picha: UNRCO/Mariam Simba)
Wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Weruweru nchini Tanzaniwa wakiwa wamebeba mabango ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kutoka namba 1 hadi 5. (Picha: UNRCO/Mariam Simba)

Mkutano huo wa siku mbili utamulika sana kuhusu utetezi na uchechemuzi, na Bi. Byanyima akiwa anatoka asasi za kiraia aliulizwa anaonaje ushirika kati yao na Umoja wa Mataifa katika kutetea malengo 17 ya maendeleo endelevu.

 “Ulimwengu kwa sasa uko katika hali ya changamoto .Tuna matatizo makubwa duniani kama vile mabadiliko ya tabianchi, pia kuongezeka kwa tofauti ya kiuchumi kati ya nchi na nchi na pia ndani ya nchi… kwa hiyo huu ni wakati wa kutetea ulimwengu ambao una sheria ambazo zimeundwa na mataifa yote ili kuona kuwa zinaheshimiwa na wote.”

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter